Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Daraja la Wami Kukamilika Julai
Mar 05, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na WUU

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage kumsimamia kikamilifu mkandarasi anayejenga Daraja la Wami na barabara unganishi kampuni ya Power Construction Corporation Limited ya nchini China ili akamilishe ujenzi huo ifikapo mwezi Julai mwaka huu.

Akizungumza mara baada kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 75.7, Prof. Mbarawa amesema kazi zilizobaki zifanyike usiku na mchana ili ujenzi huo ukamilike haraka na kwa viwango vilivvyokusudiwa.

“Daraja hili lenye urefu wa Mita 510 na barabara unganishi zenye urefu wa Kilomita 3.8, vyote vikamilike ifikapo Julai mwaka huu’ amesisitiza Waziri Prof Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa amesema Serikali itaendelea kutoa fedha kwa wakati kwa miradi yote inayoendelea nchini ili kuwawezesha wakandarasi kukosa visiingizio vya kuchelewesha miradi nchini na kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa zinazoletwa na miradi hiyo.

“Tumejipanga kuhakikisha miradi yote ya ujenzi wa barabara, madaraja na vivuko inayoendelea inakamilika kama ilivyokusudiwa, hivyo wote mliopata bahati ya kusimamia miradi hiyo fanyeni kazi kwa uzalendi ili kupata thamani ya fedha”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu kwa namna anavyowezesha miradi ya kimkakati ya WIzara ya Ujenzi na Uchukuzi kutekelezwa na kuitaja miradi hiyo kuwa ni Barabara ya Bagamoyo-Pangani Tanga hadi Lamu, Daraja la Kigongo-Busisi, barabara ya mzunguko mkoani Dodoma, Viwanja vya ndege vya Msalato, Mtwara, Musoma, Songea na Iringa ambayo ikikamilika itaibadili sura ya Tanzania kiuchumi na kijamii.

Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage amesema ujenzi wa daraja jipya la Wami lenye upana wa kuwezesha magari mawili kupishana kwa wakati mmoja utaondoa adha ya daraja la zamani lililojengwa mwaka 1959 ambalo haliendani na mahitaji ya sasa.

Mhandisi Mwambage amesema daraja jipya litapunguza ajali na msongamano katika barabara ya Chalinze hadi Segera na hivyo kuongeza tija kwa watumiaji wa barabara hiyo.

“Faida nyingine tunayoipata kutokana na mradi huu ni kuwezesha wataalam wetu kupata utaalam wa kujenga madaraja makubwa ya kiwango hiki na zaidi ya wafanyakazi 400 wamepata ajira kulipitia mradi huu”, amesema Mhandisi Mwambage.

Ujenzi wa daraja la Wami ni mwendelezo wa mikakati ya Serikali ya kufungua barabara kuu ili kuwezesha huduma za usafiri na uchukuzi kuwa za uhakika na zinazoaminika na hivyo kuvutia wawekezaji na kurahisisha huduma za uchukuzi nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi