Na Mwandishi Wetu – MAELEZO, Dar es Salaam.
Watanzania wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha ujenzi wa daraja jipya la Selander (Tanzanite) lililopo Jijini Dar es Salaam.
Pongezi hizo zimetolewa leo, Februari 1, 2022 Jijini Dar es Salaam, katika eneo la daraja jipya la Selander, ambalo limeanza kutumika leo, baada ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kuelekeza kuwa magari yataruhusiwa kupita katika daraja hilo ifikapo Februari Mosi, 2022.
“Tunaipongeza Serikali kwa kupambana na kukamilisha daraja jipya la Selander, inatia moyo tunapoona miradi mikubwa kama hii inakamilika na kutatua kero za foleni za kuingia mjini,” amesema dereva wa bodaboda, Uswege Hamza.
Uswege ameendelea kusema kuwa, katika shughuli zake za kuendesha bodaboda tatizo la foleni katika daraja la zamani la Selander lilikuwa ni kero kubwa, lakini kwa sasa, kero hiyo inaenda kutatuliwa na daraja jipya la Selander.
Kwa upande wake, Baba Mafuru amesema kuwa, Serikali imefanya kazi kubwa na nzuri, hivyo ni jukumu la sisi Watanzania kulinda rasimali hizi ili zidumu kwa muda mrefu bila kuharibiwa.
Aidha, amemshukuru Rais aliyeko madarakani na Marais wa awamu zilizopita kwa kazi kubwa walioifanya ya kuiletea Tanzania maendeleo ambayo leo hii, kila Mtanzania anajivunia nayo.
“Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hili umetuletea faraja kubwa sisi wafanyabiashara ndogondogo tunaotembeza matunda. Mimi nauza madafu, nilikuwa nakabiliana na changamoto ya msongamamo wa wafanyabiashara wengi eneo la barabara ya zamani ya Selander, hivi sasa nitahamia barabara hii” alisema Amosi Jaremiah.
Amosi aliongeza kuwa daraja hilo limeleta mwonekano mzuri wa Jiji la Dar es salaam, ambapo mwonekano waliouzoea kuuona kwenye picha kutoka nchi mbalimbali zilizoendelea, sasa wanauona ndani ya Tanzania.
Daraja jipya la Selander lina urefu wa kilomita 1.30 na barabara unganishi kilomita 5.2, limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 243.