Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

COSOTA Yasisitiza Kuzingatia Maoni ya Wadau Kanuni ya Leseni
Aug 11, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Anitha Jonas – COSOTA, Mbeya

Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) yaahidi kuzingatia maoni yaliyotolewa na Wamiliki wa Vyombo vya Habari Nyanda za Juu Kusini katika Kanuni mpya za Leseni ya Utangazaji na Maonesho kwa umma.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Mbeya na Mwanasheria wa COSOTA, Lupakisyo Mwambinga mara baada ya kueleza lengo la  kuundwa kwa Kanuni hizo na kuwapitisha wadau hao.

"Pamoja na kwamba mtakuwa mnatoa maoni kwa kuzungumza naomba pia mjaze fomu ya maoni ili tuweze kupata maoni yenu kwa njia ya maandishi, kila mmoja ajaze fomu hiyo na tutahakikisha tunazingatia maoni yote mtakayotoa,"alisema Mwambinga.

Akiendelea kuzungumza katika kikao hicho cha wadau, Mwanasheria huyo wa COSOTA alisisitiza kuwa Sheria ya Hakimiliki nchini inaeleza wajibu wa watumiaji wa kazi za muziki kulipa Mirabaha hivyo suala la ulipaji wa tozo hiyo siyo la kisiasa.

Kwa upande wa Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Alinanuswe John amewapongeza wamiliki wa vyombo vya habari  Nyanda za Juu Kusini kwa kushiriki kikao hicho, na kuwasihi wazungumze kwa hoja na waache kuwa na hasira wanapochangia hoja sababu kikao hicho kimelenga kuweka mazingira rafiki ya ulipaji wa tozo hiyo ya mirabaha.

Nae Muwakilishi wa Mmiliki wa Hekima FM, Innocent Patrick kutoka Mbinga aliiomba COSOTA kushusha tozo hiyo ya mpaka kiasi cha shilingi laki tano au laki tatu, sababu kwa sasa hali ya kiuchumi ni ngumu kutokana na wimbi la UVIKO 19.

Halikadhalika, nae Muwakilishi wa Mpanda Redio, Denis Kakala ameiomba COSOTA kuweka  aina ya muziki ambayo ikichezwa ndiyo inalipiwa huku akisema rate card za matangazo hazina uhalisia katika malipo ya matangazo yanayochezwa katika vituo vya vyombo habari. 

Katika hitimisho la kikao hicho Mwanasheria huyo alisema kuwa ameiona changamoto ya wadau hao kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu ulipaji wa mirabaha hivyo COSOTA itajipanga kuja kutoa elimu

COSOTA imeomba wadau hao katika kikao kijacho ni vyema waliyohudhuria kikao hicho ndiyo waje kikao kijacho badala ya kumtuma mtu mwingine kwani hiyo inaleta changamoto na kuanza upya kuelezana yaliokwisha kujadiliwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi