Anitha Jonas – COSOTA, Mwanza
Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) yawatoa wasiwasi wamiliki wa vyombo vya Habari Kanda ya Ziwa kwa kusema kuwa maoni yote wanayotoa kuhusu tozo ya mirabaha kwa rasimu ya Kanuni ya Leseni ya Utangazaji na Maonesho kwa Umma ya mwaka 2021 kuwa yatafanyiwa kazi.
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 11, 2021 Jijini Mwanza na Mwanasheria wa COSOTA, Lupakisyo Mwambinga katika kikao cha kukusanya maoni ya rasimu ya Kanuni ya Leseni ya Utangazaji na Maonesho kwa Umma kilicholenga kupata maoni ya tozo za mirabaha zilizopangwa kwa matumizi ya Muziki katika vyombo vya habari.
"Maoni yote tumeyapokea na tutayafikisha panapohusika na kwa wadau wa kebo tumepokea maoni yenu na changamoto zenu tutaziwasilisha ofisini ili zifanyiwe kazi na naomba mfahamu ya kuwa kikao hiki kimelenga kujenga mazingira rafiki ya tozo hii ya mirabaha iweze kulipika," alisema Mwambinga.
Akiendelea kuzungumza katika kikao hicho Mwanasheria huyo wa COSOTA alisisitiza kuwa Kanuni hiyo ni rasimu na hivyo maoni ya wadau ndiyo yataiboresha na kuifanya iweze kutekelezeka.
Pamoja na hayo nae Msimamizi wa Kituo cha Bunda FM, Revocatus Andrew aliiomba COSOTA kupunguza tozo hizo na kurudisha kiasi cha zamani ambapo walilipa laki tatu na wengine laki tano, kwani tozo ya milioni moja na nusu ni pesa nyingi kulingana na hali ya uchumi ilivyo sasa hivyo akaisisitiza taasisi hiyo kuzingatia maoni hayo wanayotoa na kuyafanyia kazi.
"Jamani biashara ya redio kwa sasa ni ngumu sana na tunajiendesha kwa tabu, hayo matangazo mnayozungumzia kwa sasa hayapatikani inafikia wakati hata pesa ya umeme wa kuendesha kituo ni changamoto halikadhalika mishahara ya wafanyakazi naomba COSOTA hili mliangalie vizuri," alisema Andrew.
Halikadhalika kwa upande wamiliki wa Kebo, Mmiliki wa Barmedas Com Ltd Hussein Hassan wa Jijini Mwanza aliomba COSOTA kushusha gharama za tozo hiyo ya mirabaha kwa Kebo televisheni kupendekeza ishushwe mpaka laki moja badala ya shilingi milioni moja na nusu iliyopendekezwa katika rasimu hiyo.