Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

China Kushirikiana na Nchi za Afrika Katika Mambo Nane
Sep 03, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na: Mwandishi Wetu, MAELEZO, Beijing-CHINA

RAIS wa Jamhuri ya Watu wa China Xi Jinping amesema, Serikali ya nchi hiyo ipo tayari kushirikiana na Afrika katika maeneo makubwa  nane katika kipindi cha  miaka mitatu ijayo itayojikita katika masuala ya viwanda, miundombinu, biashara, kilimo, ulinzi na usalama pamoja na mazingira.

Akifungua Mkutano wa Tatu wa Jukwaa la Ushirikiano wa China na Bara la Afrika (FOCAC) leo Beijing China na Rais Xi Jinping ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa hilo amesema katika masuala ya viwanda, uchumi wa Bara la Afrika na usafirishaji wa bidhaa utaendelea kupewa kipaumbele na Serikali ya China pamoja na makampuni yake yanahimizwa kuwekeza katika nchi za Afrika.

Kuhusu sekta ya kilimo, Rais Xi Jinping alisema Serikali ya China imepanga kuanzisha miradi 50 itayogharimu kiasi cha Yuan Bilioni 1 (Dola Milioni 147) itayosaidia masuala ya dharura na majanga mbalimbali ya kibinadamu sambamba na hilo, Rais Xi Jinping ameahidi kupeleka wataalamu 500 wa masuala ya kilimo ili kusaidia maendeleo ya sekta hiyo Barani Afrika.

Akizungumzia kuhusu masuala ya miundombinu, Rais Xi Jinping amesema Serikali ya China itafanya juhudi na Umoja wa Afrika kuunda mpango wa ushirikiano wa Miundombinu baina ya Bara la Afrika na China na kusaidia makampuni ya Serikali ya China kupata fursa ya ujenzi wa miradi mbalimbali.

Katika masuala ya Biashara, Rais Xi Jinping alisema  China itaongeza uingizaji wa bidhaa zinazotoka nchi za Afrika ili kuweza kuzisaidia kukuza biashara za  kimataifa na kuahidi kupunguza kodi mbalimbali za bidhaa kutoka Bara la Afrika.

Aidha Rais Xi Jinping alisema katika eneo la uhifadhi na ulinzi wa Mazingira, Serikali ya China imepanga kuanzisha miradi 50 itayosaidia mfumo wa bioanuai na ulinzi wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kulinda uifadhi wa wanyama pori.

Akifafanua Zaidi, Rais Xi Jinping alisema China pia imekusudia kuwajengea uwezo vijana wa Bara la Afrika katika mafunzo ya ufundi stadi ambapo imepanga kutoa nafasi 1000 katika hadhi ya juu, nafasi za ufadhili wa masomo 50,000 pamoja na kuwakaribisha vijana 2000 kutembelea masuala mbalimbali.

Katika eneo la afya, Rais Xi Jinping alisema Serikali ya China imepanga kuendeleza miradi 50 katika sekta ya afya, hususani vituo vinavyolenga kupunguza magonjwa mbalimbali ikiwemo ukimwi, kifua na malaria.

Kuhusu mahusiano ya mtu mmoja mmoja Rais Xi Jinping alisema Serikali ya China imepanga kuanzisha taasisi ya mafunzo kwa watu wa Bara la Afrika na kubadilishana fikra na mitazamo.

Aidha Rais Xi Jinping alisema katika Nyanja ya Amani na Usalama, China itaendelea kuweka mfuko maalum wa fedha na kusaidia Jeshi la Umoja wa Afrika ikiwemo kuanzisha miradi 50 ya kusaidia katika masuala ya kulinda amani, kupambana na uharamia na ugaidi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi