Na Mwandishi wetu- MAELEZO, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye ametoa wito kwa Wananchi wa Mkoa huo kuhamasishana ndani ya familia kuchanja chanjo ya UVIKO-19 ili kuepuka mdororo wa uchumi katika ngazi ya familia.
Andengenye ameyasema hayo mkoani Kigoma wakati akiongea na wataalamu wanaotekeleza mpango shirikishi na harakishi wa uhamasishaji na utoaji chanjo ya UVIKO-19 awamu ya pili.
“Kumekuwa na madhara kadhaa kwa wale wasiochanja na kupelekea familia zetu kutumia fedha nyingi wakati wa kuwahudumia wagonjwa hawa, kwani mgonjwa atatakiwa kuwekewa mitungi ya gesi ambayo ni gharama kubwa, ambapo kwa muda huo mgonjwa na hata anayemuhudumia hatafanya kazi, hii husababisha mdororo wa uchumi katika ngazi ya familia hivyo nawasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya UVIKO -19”, amefafanua Andengenye.
Aidha, amebainisha kuwa, katika awamu ya kwanza ya kampeni ya kuhamasisha wananchi kuchanja kulikuwa na changamoto ya muitikio katika Jamii na hivyo kujikita zaidi katika kuelimisha wananchi hao kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali ikiwemo Wanasiasa, Viongozi wa Dini, Makundi maalumu kusaidia kupeleka elimu kwa jamii ambapo ilisaidia kwa Mkoa huo.
Vilevile amewataka wakazi wa Mkoa huo kutumia sherehe za Krismasi na Mwaka mpya kwa familia kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19 kwa maslahi yao na Taifa kwa ujumla.
Nae Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Rashid Kassim amesema kuwa kampeni ya awamu ya pili ya uhamasishaji na utoaji wa chanjo umezinduliwa wakati muafaka ambapo itasaidia jamii kuzinduka kutokana na hali ya hewa iliyopo sambamba na kirusi kipya kilichoikumba Dunia wakati huu.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi wote katika ngazi za chini kuzidi kuhamasisha na kuelimisha wananchi kuhusu ugonjwa huu, pia kila mmoja kuwa Balozi wa mwenzie kwa kuhimiza wananchi kupata chanjo ya UVIKO-19
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Godfrey Smart ameeleza kuwa kwa upande wa Mkoa huo, mwezi Agosti 2021 Mkoa ulipokea chanjo za Johnson Jensen 40,000 ambapo chanjo 33,000 sawa na asilimia 92 zilitolewa kwa wananchi na chanjo 3,000 zilipelekwa katika Mkoa wa Katavi.
Ameendelea kusema kuwa, Mwezi Oktoba mkoa ulipokea chanjo 53,000 aina ya Sinopham ambapo mpaka sasa chanjo 29,000 sawa na asilimia 55 zimeshatolewa kwa wananchi, ambapo matarajio ya Mkoa ni kumaliza chanjo zote hadi kufika mwishoni mwa mwezi Disemba.
Kwa upande wake kiongozi wa timu ya uhamasishaji katika kampeni ya awamu ya pili kwa Mkoa wa Kigoma kutoka Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Bi. Nkinda Shekalaghe amewasihi watumishi wa afya kutekeleza wajibu wao kwa kufuata taratibu na miongozo ya kazi katika kutoa chanjo ya UVIKO 19 na maelekezo ya viongozi wao hata ili kuleta matokeo chanya ya UVIKO 19.
“Pamaoja na mambo mengine moja ya changamoto ya kudorora kwa zoezi la uchanjaji ni utoaji elimu ya kutosha ya UVIKO 19 kwa wananchi, hivyo nitoe wito kwenu Watumishi wa afya kutoa elimu ya kutosha bila kuchoka kwani mabadiliko ya tabia sio kitendo cha mara moja, hivyo naomba watumishi wote kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu bila kuchoka kwa wananchi ili kuleta matokeo chanya."
“Kama Watumishi wa Umma tufanye kazi kama timu,nia yetu iwe moja, kufikisha lengo la kuchanja kufikia asilimia 60% ya Watanzania”, amesisitiza Bi. Nkinda
Aidha, Nkinda ameongeza kuwa wananchi wanahitaji Wataalamu wa afya ili waweze kupata elimu na uelewa wa kutosha kuhusu chanjo, hii itasaidia kuondoa mitazamo hasi iliyopo kwa wananchi hao.