Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Changamoto za Wasanii Kushughulikiwa-Rais Samia
May 31, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na Wasanii wa muziki wa Hiphop na Bongo flava katika maadhimisho ya miaka 30 ya Msanii Bw. Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ya kuwa katika fani hiyo kwenye Tamasha la Dream Concert lililofanyika Serena Jijini Dar es Salaam.

Na Mawazo Kibamba, MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameziagiza Taasisi za Baraza la Sanaa la Taifa-BASATA na Bodi ya Filamu Tanzania kuendelea kuboresha tuzo za Wasanii kila mwaka ili kuweza kufikia viwango vya kimataifa

Pia amesema Serikali itaendelea kubuni vyanzo vya mapato ili Wasanii waendelee kunufaika na mirabaha katika msimu ujao ili kuongeza hamasa ya vijana wengi kuingia katika fani hizo.

Ameyasema hayo Mei 31, 2022 katika tamasha la Dream Concert la maadhimisho ya miaka 30 ya Msanii wa Hip Hop, Bw. Joseph Mbilinyi maarufu kama ‘Sugu’ kuwa msanii yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam yaliyoambatana na uzinduzi wa kitabu cha 'From the Streat to the Parliament’ kilichoelezea maisha halisi ya msanii huyo.

“Serikali imefanya jitihada nyingi za kuleta mageuzi katika sekta ya sanaa nchini, kwanza tulichukua uamuzi wa kuunda wizara mpya ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ili sekta yenyewe isimame kuliko ilivyokuwa mwanzo, ilikuwa imegubikwa na sekta ya habari, wizara ilikuwa na majukumu mengi na kushindwa kutoa huduma inavyopaswa, na pia tumeamua kurejesha tuzo za Wasanii wa muziki, ambazo hazikufanyika kwa miaka 7 na kuanzisha tuzo za filamu, niwaagize Wizara kupitia Bodi ya Filamu na BASATA kuhakikisha tuzo hizi zinaendelea kuboreshwa mwaka hadi mwaka tunataka zifike kwenye kiwango cha kimataifa na inawezekana kama wote tutatimiza wajibu wetu”, amesema Rais Samia.

Rais Samia pia alielezea maisha binafsi ya ‘Sugu’ akisema ni mtu mnyenyekevu na sio kama jina hilo linavyomtambulisha.

"Leo tumekutana hapa kwenye sherehe ya miaka 30 ya kuwa msanii na miaka 50 ya kuwa hapa Duniani, nikupongeze sana, wewe ni mtu mwenye majina mengi, Sugu, Mr Two, lakini mimi sitakuita Sugu maana umenyooka, Titer hayo majina ya Vijana watakuita lakini mimi ninakuita Joseph, nakuita hivyo kwa sababu mimi ni Mama na wewe ni Mtoto nimekuzaa, ukimuona Joseph unaweza sema ni Kijana Mtukutu lakini sio mtukutu, nimekuwa nae tangu Bungeni namfahamu, nakumbuka aliwahi muudhi Spika wa Bunge ikaamuriwa atolewe nje, shika mguu mkono huku wanamtoa nje unaweza sema huyu ni machachari na mtukutu na vile wanamuita sugu ila si mtukutu”,amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Msanii Sugu amesema amepitia mambo mengi mpaka kufika alipo na kumuomba Rais Samia kushughulikia changamoto za Wasanii watakazoziwasilisha kwake ili ziweze kupatiwa ufumbuzi

“Mheshimiwa Rais Wasanii tuna changamoto nyingi ambazo mimi pia nimepitia, lakini leo tumekuja kufurahi, wacha tufurahi kwanza halafu tutakuletea changamoto zetu ili zitatuliwe”, amesema Sugu.

Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Mohammed Mchengerwa amesema tangu kuanzishwa kwa wizara hiyo kumekuwa na mafanikio mbalimbali kwa Wasanii ikiwepo ya kusimamia na kuhakikisha Wasanii wanapata faida ya kazi zao, kuandaa tuzo za Wasanii na mengineyo mengi yanayolenga kunufaisha tasnia za Sanaa na michezo nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi