[caption id="attachment_34274" align="aligncenter" width="856"] Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas E Mwangela akikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Mbuyuni Wilayani Songwe, kituo hicho kilipokea shilingi milioni 400 kutoka serikali kuu na kinatarjiwa kukamilika mwezi ujao.[/caption]
Na: Mwandishi Wetu , RS-Songwe
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas E Mwangela jana jioni amehitimisha ziara yake ya siku mbili Wilayani Songwe, ambapo amekagua miradi kumi ya maendeleo na kisha kuzungumza na watumishi na watendaji wa taasisi mbalimbali zilizomo wilayani humo.
Brigedia Jenerali Mwangela akiwa ameambatana na baadhi ya maafisa wa Mkoa wa Songwe akiwemo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe wametoa maelekezo yaliyohusu kuboresha utendaji kazi kwa watumishi wa Wilaya ya Songwe.
Amesema “nimegundua kila ambacho alinieleza Mkuu wa Mkoa aliyestaafu kuhusu wilaya ya Songwe ni sahihi, upungufu alio uona nami pia nimeuona, napenda kusema mlikuwa mnamuona ni yeye Mkali ila mimi nasema alikuwa Mvumilivu”.
[caption id="attachment_34275" align="aligncenter" width="893"] Wananchi wa Kata ya Mbuyuni Wilayani Songwe wakijitolea shughuli mbalimbali za ujenzi katika Kituo cha Afya Mbuyuni ambapo serikali kuu ilitoa shilingi milioni 400 na kituo hicho kinatarajiwa kukamilika mwezi ujao.[/caption]Brigedia Jenerali Mwangela amesema hatosita kumsema na kumchukulia hatua mtendaji anayeenda kinyume na sheria na taratibu za utumishi wa umma hivyo basi watumishi hao wabadilike na kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano, watembelee na kukagua miradi inayotekelezwa wilayani humo.
Aidha amempongeza Mkuu wa Shule ya Sekodari ya Kanga wilayani humo ambapo alifanya ziara ya kushtukiza na kuwakuta walimu wote wapo darasani wanafundisha na mwalimu mkuu huyo akiwa anafundisha huku akisimamia ujenzi wa mabweni shuleni hapo, amemshauri mwalimu huyo kutumia wataalamu wa ujenzi wa wilaya ili Kusimamia ubora.
Baada ya kutembelea Daraja la Kikamba linalounganisha kata ya Kapalala na Gua, Brigedia Jenerali Mwangela amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Songwe Kumsimamia mkandarasi ili aweze kukamilisha ujenzi wa daraja hilo kwa muda uliopangwa ambao ni Septemba 7, mwaka huu.
[caption id="attachment_34276" align="aligncenter" width="1002"] Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas E Mwangela akikagua mradi wa maji Mbuyuni ambao ulikamilika mwaka 2014 lakina bado wananchi hawapati maji kutokana na maji katika chanzo hicho kuwa na rangi mbaya, Brigedia Jenerali Mwangela amemuagiza mhandisi wa maji wilayani humo kufaya utafiti wa chanzo kingine haraka.[/caption]Katika kituo cha Afya Mbuyuni amemtaka Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo kuhakikisha ujenzi unapokamilika, vifaa tiba, dawa na wataalamu wa Afya wawepo ili kituo hicho kianze kutoa huduma kwa wananchi na meneja wa Tanesco kwa kushirikiana na Mkoa kuhakikisha kituo hicho kitakapoanza kutoa huduma kiwe na umeme.
Brigedia Jenerali Mwangela amemtaka mhandisi wa maji Wilayani humo kufanya utafiti wa haraka wa chanzo kingine cha maji kwa ajili ya mradi wa maji Mbuyuni kwakuwa wananchi wamekataa kuyatumia maji ya chanzo cha awali kutokana na maji hayo kuwa na rangi mbaya.
Ameongeza kuwa wataalamu waliofanya utafiti awali hawakutendea haki taaluma yao na hivyo kusababisha hasara kwa serikali huku wananchi wakiendelea kupata kero ya maji tangu mradi huo ukamilike mwaka 2014.
Brigedia Jenerali Mwangela amemtaka Afisa Afya wa Wilaya ya Songwe kutoa elimu kwa wananchi ili wajenge vyoo bora, elimu ya masuala ya lishe, pia ahamasishe upimaji afya zao hususani kwa magonjwa yasioambukiza kama tezi dume, kisukari, VVU pamoja na kufanya tohara.
Ameongeza kwa kuwataka watunze mazingira na kuendelea kusimamia agizo la katazo la ukataji ovyo miti kwa ajili ya biashara ya mkaa, aidha ameelekeza wananchi wanaruhusiwa kuvuna miti katika maeneo maalumu yaliyotengwa na wakala wa huduma za misitu (TFS).
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Mathias Nyange amewataka watumishi kuacha utoro kwakuwa wengi wao ifikapo siku ya ijumaa hutoroka na kuelekea Mkoa wa jirani walipoweka makazi yao.
RPC Nyange amesema, “nitamshauri Mkuu wa Mkoa vikao viwe vinafanyika siku ya Jumamosi ili kufuta utoro huu, nawashauri watumishi unapopangiwa kituo cha kazi ndio kwenu papende, ufanye kazi kwa bidi”.
Ameongeza kuwa serikali inatukanwa kutokana na uzembe wa baadhi ya watumishi hivyo wajitume wabadilike na wafanye kazi kwa ushirikiano hasa katika kumsaidia mwananchi masikini apate maendeleo.