Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

BOT Ina Fedha Za Kigeni Za Kutosha
Nov 20, 2018
Na Msemaji Mkuu

Benki Kuu ya Tanzania (BOT), imesema ina kiwango kikubwa cha fedha za kigeni kinachoweza kutosheleza kulipa madeni ya serikali na kutoa huduma zingine katika kipindi cha miezi mitano ijayo.

Hayo yameelezwa Novemba 20 na Gavana wa Benki kuu Profesa Frolence Luoga ,alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari mjini Arusha akitoa ufafanuzi kuhusu oporesheni iliyoendeshwa Juzi na benki hiyo dhidi ya maduka ya kubadilisha fedha jijini Arusha.

Gavana,amesema  zoezi hilo liliratibiwa na kitengo cha ukaguzi cha benki kuu katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria na ni zoezi la tatu kufanyika nchini.

Uchunguzi wa kina katika kipindi cha miezi sita iliyopita ulibaini kuongezeka kwa biashara ya kubadilisha fedha kinyume cha sheria na kukua kwa biashara haramu ya fedha za kigeni na utakatishaji wa fedha hususani kupitia maduka ya kubadilisha fedha jambo ambalo ni hatari kwa uchumi wan chi.

Juhudi za benki hiyo kuwapata wahusika hazikuzaa matunda katika oporesheni mbili zilizopita kwa sababu iligundulika kulikuwepo na mtandao mpana na madhuhuti wa shughuli hizo ambao ulilenga kukwamisha shughuli za udhibiti .

Baada ya mashauriano na wataalamu na kushirikiana na vyombo vya upelelezi na usimamizi ilionekana kuwa ili kufanikisha zoezi lililokusudiwa  ni muhimu wahusika wote kudhibitiwa kwa wakati mmoja na kufanyiwa ukaguzi jambo  lilihitaji ushiriki wa maofisa kutoka vyombo vya dola .

Amesema zoezi hilo limeshirikisha askari wa jeshi la wananchi na jeshi la polisi na kuzuia watu wasiingie ndani ya maduka hayo kufanya miamala ya kifedha na zoezi hilo limemalizika salama bila kuathiri mtu yeyote.

Gavana,amesema katika kipindi cha miezi mitatu ,Benki kuu imesitisha utoaji wa leseni za biashara ya ubadilishaji fedha na maombi yote mapya yamesitishwa na  hayatapokelewa.

Gavana, amesema wale wote watakaopatikana na hatia watafikishwa mahakamani,leseni zao zitafutwa na hawataruhusiwa kufanya biashara hiyo tena na Benki haitoa taarifa wakati kesi zao zikishughulikiwa kisheria ili kutokuingilia uhuru wa mahakama.

Amesema watakaopatikana na tuhuma kwenye oporesheni mbili zilizopita na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria wanatakiwa kuzirejesha leseni zao benki kuu mara moja pia zitasitishwa mpaka kesi zao zitakapokamilika.

Aidha uchunguzi uliofanyika umebaini waendeshaji wengi wa maduka ya kubadilishia fedha hawakukidhi vigezo vyote japo leseni zilitolewa kwao baada ya taarifa zao kupotoshwa wote watapewa notisi ya kusitisha leseni na maduka yao kufungwa ambapo yeyote anayejua kuwa upatikanaji wa leseni yake una dosari anashauriwa kurejesha leseni hiyo kwa hiari.

Wale ambao wanatumia leseni ambazo sio zao wanatakiwa kufunga maduka hayo mara moja kabla mkono wa sheria haujawafikia ili kuzuia wasio stahili kupenyeza na kujipatia leseni za biashara ya kubadilisha fedha.

Jana jiji la Arusha lilikumbwa na taharuki baada ya maduka ya kubadilisha fedha kuzingirwa na askari wa jeshi la wananchi na polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi