Timu ya wataalam kutoka Uganda na Tanzania wakiwa eneo linalofanyiwa tafiti ya uwezekano wa uwepo wa mafuta,timu hiyo inaongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (Tanzania) na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini (Uganda), Robert Kasande
Na Mwandishi Wetu
Imeelezwa kuwa miamba iliyo katika Bonde la Eyasi Wembere hususan mabonde madogo (sub basin) ya Wembere na Manonga yaliyopo katika mikoa ya Tabora, Shinyanga, Singida na Simiyu inawezekana kuwa na mafuta kutokana na sifa zake za Kijiolojia na Kijiofizikia.
Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini (Uganda), Robert Kasande na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini (Tanzania), Dkt Mhandisi Juliana Pallangyo katika Mkutano na Wananchi uliofanyika katika kijiji cha Mwashiku wilayani Igunga mkoani Tabora. Mkutano huo uliandaliwa na Mkuu wa mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry.
Viongozi hao walitoa kauli hiyo baada ya timu ya wataalam kutoka Uganda na Tanzania kufanya ziara katika Bonde hilo hususan mabonde madogo ya Wembere na Manonga na kutembelea miamba inayoonekana katika maeneo ya Sekenke mkoani Singida, na vijiji vya Mwanzugi na Kining'inila mkoani Tabora.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda alieleza kuwa baada ya kuona dalili hizo Timu hiyo itatoa mapendekezo mbalimbali kwa Wataalam wa Tanzania ili kuweza kufikia lengo la Serikali la kuchimba Mafuta katika Bonde la Eyasi na Ziwa Tanganyika .
Alisema kuwa endapo Mafuta yatapatikana katika Bonde hilo yataweza kusafirishwa katika Bomba la Mafuta linalotoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga na kuweza kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Aliongeza kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa Tanzania kugundua mafuta katika Bonde hilo kwani nchini nyingine ambazo Bonde hilo linapita kama Kenya na Uganda tayari wamegundua Mafuta. Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo alisema kuwa kupatikana kwa mafuta katika eneo hilo kutaimarisha hali ya uchumi nchini na kuwaasa wananchi kujiandaa na fursa za kiuchumi ikiwemo utoaji wa huduma mbalimbali wakati wataalam wakiwa wanafanya shughuli mbalimbali za kitafiti katika eneo husika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry aliwataka wananchi wanaozunguka Bonde hilo na Viongozi wa Serikali katika Mkoa huo kutoa ushirikiano kwa wataalam watakaofanya kazi za kitafiti ili zoezi hilo liweze kufanyika kwa ufanisi.
Naye, Mjiofizikia kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli, (TPDC), Sindi Maduhu alisema kuwa bonde hilo la Eyasi Wembere lina ukubwa wa Kilomita za mraba 19,197 likiwa na takwimu za awali za kijiofizikia (Airborne gravity gradiometry) zilizokusanywa na kutafsiriwa mwaka 2015/2016.