Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Bodi ya Usajili ya Wahandisi inatarajia kuadhimisha Siku ya Wahandisi Tanzania inayotarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 5 hadi 7 mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee uliopo jijini Dar es salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo jijini Da es salaam, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya miaka 50 ya Bodi ya Wahandisi, Mhandisi Ngwisa Mpembe alisema kuwa Jumuiya ya Wahandisi Tanzania itaadhimisha Siku ya Wahandisi kwa mara ya 16, sambamba na Maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Bodi hiyo.
Aidha, Mhandisi Mpembe alitaja baadhi ya malengo ya kuadhimisha Siku ya Wahandisi kuwa ni kuiwezesha jumuiya ya kihandisi kuuonyesha umma mambo ambayo wahandisi wa Tanzania wanaweza kufanya katika kuleta maendeleo ya nchi.
Alibainisha malengo mengine kuwa ni “kuuwezesha umma kutambua michango tunu inayofanywa na wahandisi wa Tanzania katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini, kuwatia moyo wanafunzi wa kitanzania wanaosomea uhandisi ili wafanye vizuri zaidi katika masomo yao, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha waajiri wa wahandisi na watumiaji wa huduma za kihandisi kutambua uwezo wa wahandisi wazalendo na kampuni au mashirika ya ushauri ya kihandisi ya kizalendo, ”alisema Mhandisi Mpembe.
Maadhimisho ya 50 na Siku ya Wahandisi mwaka huu yatajumuisha shughuli mbalimbali kama vile majadiliano ya kitaaluma, kiapo cha wahandisi, maonesho mbalimbali ya kiufundi na biashara, pamoja na kutoa tuzo kwa wahandisi na waliosaidia uhandisi ndani ya miaka 50.
Naye kwa upande wake, Kaimu Msajili, Bodi ya Usajili ya Wahandisi, Mhandisi Patrick Barozi alitoa wito kwa watanzania kuja katika maonesho hayo ambapo alisema “kutakuwa na maonesho mbalimbali ya kiteknolojia , mfano kutengeneza barabara kwa kutumia mabaki ya plastiki”
Katika maadhimisho hayo ya siku tatu yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, mashirika ya umma, na binafsi, na wageni kutoka nchi za Zambia, Nigeria, Ghana, Uganda, Ethiopia, Rwanda, Misri, Malawi na Kenya.