[caption id="attachment_36727" align="aligncenter" width="750"] Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Mhe. Augustino Mrema akizungumza na Wafungwa wanufaika wa Parole na wanaoendelea kutumikia vifungo vyao katika mpango wa Parole[/caption]
Na Lucas Mboje, Dodoma;
BODI ya Taifa ya Parole imetembelea Gereza Kuu Isanga Dodoma na kufanya mazungumzo na baadhi ya wafungwa wanaoendelea kutumikia vifungo vyao chini ya mpango wa Parole kabla ya kutembelea wafungwa wanufaika wa mpango huo waliopo Mkoani Dodoma ili kuona maendeleo yao baada ya kupitia programu mbalimbali za urekebishaji magerezani.
Bodi ya Taifa ya Parole imetumia nafasi hiyo leo Oktoba 12, 2018 kutoa ushauri kwa wafungwa wa Parole nchini huku ikiwataka kuishi vyema katika jamii katika kipindi chote wanachoendelea kutumikia vifungo vyao katika mpango huo na baada ya kumaliza vifungo hivyo wawe raia wema katika jamii.
Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Mhe. Augustino Mrema amewaasa wafungwa hao kuhakikisha kuwa wanaishi kwa kutii sheria za nchi na hivyo kuwa raia wema.
[caption id="attachment_36728" align="aligncenter" width="750"] Wafungwa wanufaika wa Parole na wanaoendelea kutumikia vifungo vyao katika mpango wa Parole wakimsilikiza Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Mhe. Lyatonga Mrema[/caption]“Nafahamu mnazo changamoto mbalimbali mnazokumbana nazo wakati bado mnatumikia vifungo vyenu kwenye jamii ikiwemo kunyanyapaliwa, nawasihi sana msijiingize katika uhalifu badala yake fanyeni kazi halali za kujiingizia kipato”. Alisema Mhe. Mrema.
Aidha, Wajumbe wa Bodi hiyo pia walipata fursa ya kuwatembelea baadhi ya wafungwa wanufaika wa mpango huo ambao wanajishughulisha na kazi za ujenzi wa nyumba za makazi jijini Dodoma baada ya kunufaika na programu mbalimbali za urekebishaji walipokuwa magerezani.
Naye, Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike ambaye pia ni Katibu wa Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya Parole ametoa wito kwa jamii kuwa na mtizamo chanya kuhusu wafungwa wanaotoka magerezani kwani Jeshi la Magereza hujiridhisha na kiwango cha mfungwa kujirekebisha.
[caption id="attachment_36729" align="aligncenter" width="750"] Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike ambaye ni Katibu wa Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya Parole akitoa utambulisho mfupi kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Mhe. Augustino Mrema(katikati meza kuu) azungumze na baadhi ya wafungwa wanufaika wa mpango wa Parole(hawapo pichani) leo Oktoba 12, 2018 katika Bwalo la Gereza Kuu Isanga, jijini Dodoma. Kulia ni Kamishna wa Magereza - Huduma za Urekebishaji, Agustino Mboje.[/caption]“Jamii iwe na mtizamo chanya kwa kuwakubali na kuwapokea wafungwa wanaotoka magerezani ili wajiunge nao katika jamii kama watu wengine”. Amesisitiza Jenerali Kasike.
Kwa upande wao wafungwa wanaoendelea kutumikia vifungo vyao katika mpango huo wa Parole wameelezea baadhi ya changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo ikiwemo kunyanyapaliwa na jamii, ukosefu wa mitaji ya kuanzisha biashara, n.k.
Mpango wa Parole upo chini ya Sheria ya Bodi za Parole iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na utekelezaji wa Sheria hii ulianza rasmi mwaka 1999 na kufanyiwa marejeo mwaka 2002.
Tangu kuanzishwa kwa sheria hii jumla ya wafungwa 5773 wamejadiliwa. Kati ya wafungwa hao, wafungwa 5082 wamenufaika kwa mpango wa Parole na wafungwa 691 hawakunufaika kwa kukosa sifa.