Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, ameielekeza Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kubuni mikakati madhubuti ya kukuza uchumi wa viwanda kupitia rasilimali za misitu na nyuki, kuongeza mashamba ya miti na kuimarisha usimamizi wa misitu nchini.
Akizindua Bodi hiyo Februari 13, 2026 jijini Dodoma, amesema sekta ya misitu na nyuki ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa na inaweza kuwa chachu ya maendeleo ya viwanda iwapo itawekewa mikakati madhubuti ya uzalishaji na uongezaji thamani.

Amesema pamoja na mafanikio yaliyofikiwa na TFS katika usimamizi wa rasilimali hizo, bado ipo haja ya kuongeza juhudi ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa.
Dkt. Kijaji amesema TFS imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuimarishwa kwa mifumo ya kiutendaji na utoaji wa huduma, kuongezeka kwa kasi ya upandaji miti na urejeshaji wa maeneo yaliyoharibika, kupanuka kwa hifadhi za misitu ya asili, kudhibiti uvamizi wa misitu pamoja na kuongezeka kwa mapato ya Serikali.
.
Waziri Kijaji, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha sekta ndogo ya nyuki kwa kuongeza uzalishaji wa asali, nta na mazao mengine ya kibiashara, pamoja na kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao hayo.
Aidha, ameitaka Bodi hiyo kusimamia uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata asali hususan katika mikoa yenye uzalishaji mkubwa ili kuongeza thamani na soko la bidhaa hiyo

“Nataka juhudi za makusudi ziwekwe kuongeza kasi ya ufugaji wa nyuki na uzalishaji wa mazao yake. Nyuki wakitumika vizuri wataongeza kipato kwa jamii zinazozunguka misitu na hivyo kupunguza utegemezi unaochochea uharibifu wa misitu,” amesema.
Ameongeza kuwa rasilimali nyuki zina manufaa ya kiuchumi na kimazingira, zikiwemo kusaidia kudhibiti wanyama waharibifu wa mazao kwa njia ya kibailojia.

Kwa upande wake Bi. Neema Msomba akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Hazina, amewapongeza wajumbe wa Bodi kwa kuaminiwa kusimamia taasisi hiyo muhimu na kuahidi ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha TFS inafikia malengo yake.

Amesema Bodi hiyo tayari imepatiwa mafunzo ya usimamizi madhubuti ili kuimarisha uendeshaji wa Wakala na kuongeza mchango wake katika Mfuko Mkuu wa Serikali.