Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imejipanga kuanzisha miradi ya kimkakati ya miundombinu ya kutolea huduma za ubingwa wa juu, ili kuendelea kuboresha na kuongeza wigo wa wananchi wengi kupata matibabu ndani ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi ameyasema hayo leo Machi 04, 2025 katika ukumbi wa Idara ya Habari- MAELEZO jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya hospitali hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ikiwa ni program iliyoandaliwa na Idara hiyo.
“BMH imeendelea kuanzisha miradi itakayosaidia kuboresha huduma za ubingwa wa juu, ikiwemo mradi wa upanuzi wa huduma za upandikizaji figo wenye thamani ya shilingi bilioni 3.7 ambapo utaongeza idadi kufikia wastani wa watu wanne kwa mwezi kutoka watu wawili, na kuanza kwa ujenzi wa kituo cha matibabu ya kansa chenye thamani ya shilingi bilioni 30.8 ambao utasogeza huduma kwa wananchi milioni 14 na kupunguza rufaa kwenda Dar es Salaam au nje ya nchi”, amesema Prof. Makubi.
Pia, amesema kuwa BMH imefanikiwa kuongeza vyumba vitatu vya upasuaji vyenye thamani ya shilingi milioni 250 ambavyo vitasaidia kufanyika kwa oparesheni 50 kwa siku kutoka 30, hatua itakayopunguza muda wa wagonjwa kusubiri kufanyiwa upasuaji pamoja na kusimika mtambo wa kuzalisha hewa tiba wenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 wenye uwezo wa kuzalisha mitungi 400 kwa saa 24.
Katika kipindi hicho cha miaka minne, hospitali hiyo imeanzisha Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi kwa ngazi ya Stashahada ni chuo cha kwanza kutumia mtaala chini ya NACTVET kwa kozi ya radiographia na uchunguzi wa magonjwa hapa nchini.
Kwa upande mwingine, Prof. Makubi amesema BMH imepanua diplomasia ya afya na taasisi za ndani na nje ya nchi ambapo imekuwa na ushirikiano na wadau wa ndani kama vile UDOM, Muhimbili, KCMC na Bugando, na wadau kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani.
Wadau hao wa nje ni Tokushukai Medical Group – Japan katika kujenga uwezo wa upandikizaji figo, Help 3 Monza –Italy-kujenga uwezo wa kupandikiza uloto, Pathology Without Boarder–Italy, Childrens Heart Charity Association – Kuwait, Zgt-Overzee Foundation – Netherland.
Akiongelea kuhusu uelekeo wa hospitali hiyo, Prof. Makubi amesema kuwa wamepanga kupandisha hadhi hospitali kufikia kiwango cha Hospitali ya Taifa, kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika kuboresha huduma ikiwepo matumizi ya akili unde (AI) katika huduma za kusaidia wauguzi, huduma kwa wateja, ‘robotic surgeries’, upasuaji wa matundu na kukamilisha miradi ya mkakati ya miundombinu inayoendelea, kujenga vituo vya umahiri vya upandikizaji figo (Japan), Uloto (EAC), upasuaji wa moyo, upasuaji ubongo, masikio, pua na koo (ENT), mama na mtoto na tiba ya macho.