Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bilioni 52 Zakamilisha Ujenzi Nyumba 644 Magomeni Kota
Mar 23, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Ahmed Sagaff – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 51 zilizoendeleza na kukamilisha mradi wa ujenzi wa nyumba 644 za makazi za Magomeni Kota jijini Dar es Salaam ambao ni sehemu ya juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuboresha makazi na nyumba za wananchi.

Hayo yamesemwa leo (Machi 23, 2022) na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla kwenye uzinduzi wa nyumba hizo zilizopo eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam.

“Ulipoingia madarakani mradi huu ulikuwa haujakamilika lakini ulielekeza na kutoa fedha ambazo zimekamilisha mradi huu shilingi bilioni 51, hongera sana Mhe. Rais,” amesema Mhe. Makalla.

Sambamba na hilo, kiongozi huyo amearifu kuwa Magomeni Kota yenye nyumba 644 ndio makazi yenye wakazi wengi Tanzania yakifuatiwa na yale ya Michenzani, Zanzibar yaliyoasisiwa na Hayati Abeid Amaan Karume.

“Mheshimiwa Rais, uzinduzi wa nyumba hizi 644 ni utekelezaji wa ahadi yako ulipopewa nafasi ya kuwatumikia Watanzania, ulisema kwamba utahakikisha unaendeleza miradi yote iliyoachwa na mtangulizi wako Dkt. John Pombe Magufuli, na hapa umethibitisha kwa vitendo,” amehabarisha Mhe. Makalla.

Aidha, Mhe. Makalla amesema ujenzi huo umetumia ekari tisa kati ya ekari 32 zilizokwepo na kwamba eneo lililobakia litatumika kujenga soko na pia sehemu nyingine itakuwa viwanja vya michezo.

Mradi wa Magomeni Kota ulioanza Oktoba Mosi, 2016 umegharimu takriban shilingi bilioni 52.2 ukihusisha ujenzi wa majengo matano yenye ghorofa nane na tisa ambapo nyumba zilizokwepo hapo awali zilikuwa za kawaida.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi