Bilioni 25.7 kutumika kutekeleza miradi ya maji taka inayowanufaisha wananchi wanaokadiriwa kufikia milioni 1.8 katika jiji la Dar es Salaam.
Akieleza kwa Waandishi wa Habari leo Agosti 11, 2023 jijini Dodoma kuhusu mafanikio na utekelezaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Bw. Kiula Kingu amesema miradi hii ni ya kisasa na katika mfumo wake wa uchakataji majitaka itatoa gesi asilia kwa ajili ya kupikia, itatoa mbolea itakayoweza kutumika katika kustawisha bustani za miti na majani lakini pia maji yatakayochakatwa yataweza kutumika kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji, usafishaji wa barabara na mitaro ama kupoozea mitambo.
“Utekelezaji wa Miradi ya Usafi wa Mazingira kuboresha afya na mazingira Pamoja na kuwekeza nguvu katika utoaji wa huduma za majisafi, DAWASA imejipanga kikamilifu na kuchukua hatua za makusudi za kuboresha usafi wa mazingira kupitia miradi mikubwa na midogo”, alisisitiza
Akieleleza zaidi amesema hii ni kwasababu upatikanaji wa maji unapoongezeka unapaswa uambatane na usimamizi madhubuti wa usafi wa mazingira katika Wilaya ya Kinondoni na Ilala, miradi ya kuchakata majitaka itajengwa maeneo ya Mbezi Beach na Buguruni.
Mradi wa Mbezi Beach unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Benki ya Dunia ambapo jumla ya shilingi bilioni 132.3 zitatumika kujenga mtambo wa kisasa wenye uwezo wa kuchakata lita milioni 16 kwa siku.
Aidha, alieleza kuwa mradi mwingine ni wa kujenga mfumo wa kukusanya majitaka na maeneo nufaika katika awamu hii ni Mbezi beach, Kilongawima, baadhi ya maeneo ya Kawe na Salasala. Utekelezaji wa mradi umeanza na Wakandarasi wanaendelea na shughuli za maandalizi ya ujenzi.
Sanjari na hilo DAWASA pia imekuja na ubunifu wa kujenga mifumo na mitambo midogo midogo ya kuchakata majitaka inayojengwa maeneo ya pembezoni ambapo zaidi ya lita 780,000 za majitaka zitakuwa zikichakatwa kwa siku.
Miradi hii ambayo pia itajumuisha ujenzi wa vyoo vya umma 30, itasaidia kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma hizi muhimu na hivyo kuboresha usafi wa mazingira. Aidha miradi hii itasaidia wananchi kupata huduma za usafi wa mazingira kwa gharama nafuu karibu na maeneo wanayoishi. Wakandarasi wanaotekeleza miradi wanaendelea na ujenzi.
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuwezesha dhana ya usafi wa mazingira kutekelezwa kwa vitendo katika jiji la Dar es Salaam.