Na. Alfred Mgweno (TEMESA Mwanza)
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) imekamilisha mradi wa ukarabati wa vivuko viwili vinavyotoa huduma mkoani Mwanza kwa gharama ya shilingi Bilioni 2.9.
Vivuko hivyo vya MV. SENGEREMA na MV. TEGEMEO, vimefanyiwa ukarabati mkubwa baada ya kufikia muda wake wa kufanyiwa ukarabati ambayo imekuwa ni desturi inayofanywa na Wakala huo mara kwa mara ili kuhakikisha vivuko hivyo vinaendelea kutoa huduma bora wakati wote vikiwa katika hali ya usalama.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika hafla fupi za kupokea vivuko hivyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mhandisi Japhet Maselle amesema kivuko cha MV. SENGEREMA kilibainika kuwa na uchakavu mkubwa zaidi na hivyo kupelekewa kutolewa kwenye maji kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati mkubwa mapema iwezekanavyo.
‘‘Kivuko kilipotolewa kwenye maji ili kazi ya ukarabati ianze kilibainika kuwa na uchavu mkubwa zaidi, hivyo kupelekea kuandaa mapitio mapya yaliyopelekea kivuko kufungwa injini mbili mpya pamoja na propulsion unit mbili mpya zilizogharimu jumla ya shilingi 1,809,956,662.92. Mabadiliko ya mkataba huu yalifanya kazi ya ukarabati kuanza rasmi Aprili 22, 2020 kwa gharama ya shilingi 2,249,181,662.92‘‘. Alisema Mhandisi Maselle
‘’Vile vile kivuko hiki kimewekewa vifaa vya kisasa vya kukiongoza kama Radar, GPS, Magnetic Compass, vifaa vya mawasiliano na vifaa vya uokoaji vya kutosha kwa watu wazima na watoto ambavyo ni makoti ya kujiokoa na maboya ’’. Alimalizia Mtendaji Mkuu.
Akitoa taarifa hiyo kwa Waandishi wa Habari, Mhandisi Maselle amesema kampuni ya kizalendo ya M/S SONGORO MARINE TRANSPORT LTD ya jijini Mwanza ilishinda zabuni ya ukarabati wa kivuko hicho kwa gharama ya shilingi 672,417,900.00 za Kitanzania ambapo ilianza kazi hiyo mara moja ili kuhakikisha wananchi wanaotegemea kivuko hicho wanakipata baada ya muda mfupi zaidi.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Songoro, Major Songoro akizungumza katika hafla hiyo fupi ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuiamini na kuipa zabuni za kutengeneza na kukarabati vivuko na kuahidi kuendelea kufanya kazi yenye viwango na ubora uliotukuka.
Kivuko cha MV. SENGEREMA kina uwezo wa kubeba abiria 490 na magari 24 sawa na tani 170, kina urefu wa mita 55, upana wa mita 10.5 na kina cha kuelea mita 1.4, wakati Kivuko MV. TEGEMEO kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 sawa na tani 85, urefu wa mita 37, upana wa mita 10 na kina cha kuelea mita 0.75.
Fedha zote zilizotumika kukarabati vivuko hivyo zimetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.