Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bilioni 175 Zalipa Madeni ya Wazabuni Wizara ya Ulinzi na JKT
Mar 15, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Georgina Misama – MAELEZO, Dar es Salaam.

Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 175 kwa ajili ya kulipa madeni ya wazabuni walitoa huduma mbalimbali katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Akizungumza leo katika mkutano na Waandishi wa Habari uliohusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena Tax alisema kwamba kupatiwa fedha hizo kumeiwezesha Wizara kujenga imani kwa watoa huduma wake.

Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita , Wizara imewezeshwa kulipa madeni yenye thamani ya zaidi ya shilingi billioni 175 kwa wazabuni waliotoa huduma mbalimbali ambapo imejenga imani kwa serikali na kuiwezesha wizara kuendesha majukumu yake ya msingi kwa ufanisi”, alisema Dkt. Tax.

Kwa upande mwingine Wizara imeweza kushughulikia migogoro ya ardhi ipatayo 74 iliyohusisha mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Chukwani Dar es salaam, Dodoma, Kagera, Kigoma, Lindi na Mara. Mikoa mingine ni pamoja na Morogoro, Mwanza, Njombe, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga na Singida ambapo zoezi hilo linaendelea kwenye maeneo mengine nchini ambayo bado hayajafikiwa.

Aidha, katika kipindi cha mwaka mmoja, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limewezeshwa kutoa mafunzo mbalimbali ya kijeshi katika shule na vyuo vya kijeshi ndani na nje ya nchi sambamba na kuendesha mafunzo ya Ulinzi na Stratejia ya muda mrefu na mfupi kwa maafisa wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na watumishi wa Umma.

Kwa upande wa mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Jeshi hili, Dr Tax alisema ujenzi huo unaendelea vizuri na kwa hatua ulipofikia unatarajia kukamilika ifikapo June 2022.

Serikali ya Awamu ya Sita imeiwezesha Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuendelea na ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa huko Kikombo Dodoma. Ujenzi huo unaotekelezwa kwa kutumia rasilimali fedha, na wataalamu wa ndani umefikia asilimia 70 na unatarajia kukamilika ifikapo June 2022”, aliongeza.

Dkt. Tax ametoa wito kwa watanzania wote kuendelea kudumisha amani na utulivu, kwa ustawi wa Taifa na wananchi wake, kwani kila Mtanzania anaowajibu wa kulinda amani ya Taifa kwa ustawi wa Taifa na manufaa ya wote.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi