Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bilioni 10 Kufanikisha Mradi wa Kusambaza Mitungi ya Gesi
Aug 18, 2023
Bilioni 10 Kufanikisha Mradi wa Kusambaza Mitungi ya Gesi
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy akizungumza na Waandishi wa Habari leo Agosti 18, 2023 kuhusu utekelezaji wa majukumu ya wakala hiyo na mwelekeo kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 katika Ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma
Na Mwandishi Wetu

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 imetenga  shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kufanikisha mradi wa kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo Agosti 18, 2023 katika Ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya wakala hiyo na mwelekeo kwa mwaka wa Fedha 2023/24.

“Wakala umeanza kutekeleza mradi wa kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia kwa utaratibu wa utoaji ruzuku kuwezesha usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) 71,000  yenye thamani ya shilingi bilioni 3 pamoja na majiko banifu 200,000   katika maeneo ya vijijini,” amebainisha Mhandisi Hassan.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Gesi Asilia (CNG) amesema wakala umeanza kusambaza gesi asilia ya kupikia katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani (Pembezoni mwa Mkuza wa Bomba Kuu la Kusafirisha Gesi Asilia) ambapo utekelezaji wa mradi huo utahusisha wakala pamoja na TPDC.

“Kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 jumla ya shilingi bilioni 20 zinatarajiwa kutumika katika  mradi huu ambao  utahusisha ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi asilia (CNG) lenye urefu wa km 44.4 (Mnazi Mmoja – Lindi (km 22.9) na Mkuranga – Pwani (km 21.5)) ambapo jumla ya nyumba/wateja 980 kunufaika (Mnazi Mmoja – Lindi, wateja 451 na Mkuranga-Pwani, wateja 529),” amefafanua Mhandisi Hassan.

Mbali na hayo, Serikali kupitia REA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imetenga Dola za Kimarekani (USD Milioni 6) kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa majiko banifu ya kupikia ambapo takribani Majiko 200,000 yanatarajiwa kusambazwa katika maeneo mbalimbali ya vijijini na vijiji miji Tanzania Bara.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi