Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Benki ya Dunia Yaipongeza Tanzania kwa Kusimamia Vizuri Uchumi Wake
Oct 18, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Benny Mwaipaja, Washington, DC


Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, ameipongeza Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mageuzi makubwa kwenye uchumi.


Bi. Kwaka ametoa pongezi hizo Jijini Washington D.C nchini Marekani alipokutana kwa ajili ya kuagana na ujumbe wa Tanzania, ulioshiriki mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.


Alisema kuwa uchumi wa Tanzania umekuwa tulivu na umekua kwa kasi wakati nchi mbalimbali duniani zikihaha kujikwamua kiuchumi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo msukosuko wa uchumi unaotokana na vita ya Urusi na Ukraine Pamoja na madhara ya UVIKO-19.


Aliipongeza pia Tanzania kwa kuwa na sera nzuri za fedha na uchumi zinazoleta utulivu kwenye uchumi na kufanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei akieleza kuwa wakati nchi mbalimbali zikihangaika na janga la mfumuko wa bei wa tarakimu mbili, akitolea mfano wa nchi ya Ghana ambayo mfumuko wa bei umefikia asilimia 30, wakati Tanzania imeweza kuwa na mfumuko wa bei wa tarakimu moja tu ambayo ni asilimia 4.8.


Makamu huyo wa Rais wa Benki ya Dunia alisema kuwa mfumuko wa bei ni kama kodi mbaya inayowaumiza zaidi wananchi masikini na kwamba Benki yake itaichukua Tanzania kama kielelezo na mfano wa kuigwa na nchi nyingine duniani.


“Kwenye nchi nyingi tumeshuhudia akiba dhaifu ya fedha za kigeni, lakini ni tofauti kwa Tanzania ambapo mna akiba ya fedha za kigeni inayotosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje za kipindi cha takribani miezi mitano, hali kadhalika tumeshuhudia nakisi ya bajeti kwenye nchi nyingine lakini Tanzania nakisi yenu ni asilimia 3.5 pekee ya Pato la Taifa. Jambo hili ni la kupongezwa”, Alisema Bi. Kwakwa


Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliishukuru Benki ya Dunia kwa pongezi hizo kwa usimamizi mzuri wa sera za uchumi na fedha na kuahidi kumfikishia pongezi hizo Mheshimiwa samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Aidha, Dkt. Nchemba alirejea kutoa shukrani zake kwa Benki hiyo kwa msaada mkubwa wa ushauri wa kitaalam na rasilimali fedha, vinavyochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi na hivyo kupunguza umasikini wa watu wake.


Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango - Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Salum Mkuya pamoja na Maafisa wengine waandamizi kutoka Tanzania na Benki ya Dunia. 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi