Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Benki ya Dunia Yaahidi Kutoa Fedha Kukuza Matumizi ya Sayansi na Teknolojia Tanzania
Oct 10, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na.WFM Mjini Bali- Indonesia

Benki ya Dunia imeahidi kuwekeza zaidi nchini Tanzania katika Sayansi na  Teknolojia ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi  kwa lengo la kuisaidia Tanzania kukuza uchumi wa viwanda na kuondoa umasikini  kwa wananchi wa wake.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango, alipofanya mkutano na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem, katika mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Mjini Bali Indonesia.

Dkt. Mpango amesema kuwa Benki ya Dunia imeamua kuwekeza katika teknolojia kwa kuwa ni eneo sahihi linaloweza kukuza uchumi wa Taifa kwa zaidi ya mara mbili kutokana na tafiti zilizofanywa na Benki ya Dunia.

“Kimsingi Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia amefurahia ajenda za maendeleo za Tanzania kuhusu kujenga uwezo wa rasilimali watu katika kukuza uchumi wa viwanda na ameahidi kuanza kwa kuwekeza zaidi kwa watoto wenye umri mdogo ili mipango ya maendeleo ya nchi iwe endelevu”, alieleza Dkt. Mpango.

Aidha Waziri Mpango alimueleza Makamu wa Rais wa Benki hiyo kuwa Tanzania imeweka  mikakati  mbalimbali ya kujenga uchumi wa viwanda utakaotumia malighafi za ndani ili kuongeza ajira kwa wananchi walio wengi.

Kuhusu umuhimu wa Sekta Binafsi katika maendeleo ya nchi Waziri Mpango alisema Makamu wa Rais Bw. Ghanem, ameahidi kuwekeza zaidi katika miradi ya pamoja kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), kwa kuiwezesha Serikali ya Tanzania na wadau wengine kwenda kupata mafunzo yatakayoongeza ujuzi wa utekelezaji wa miradi hiyo katika nchi zilizofanya vizuri katika eneo hilo ili kuongeza ufanisi wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.

Kwa upande wake Kamishna na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere, amesema kuwa mfumo wa dunia ya sasa unazitaka nchi kujitegemea kimapato hivyo TRA itaendelea kuongeza nguvu ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa  kuwa Benki ya Dunia imeahidi kuboresha miundomibnu ya ukusanyaji mapato kwa nchi ya Tanzania.

Waziri Mpango ameiomba Benki ya Dunia iendelee kuisaidia Tanzania kwa kutoa rasilimali fedha katika kuwezesha miundombinu ya kukuza uchumi ikiwemo ya miradi ya nishati ya umeme, ujenzi wa reli kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), na miradi ya maji.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia ameahidi kutembelea Tanzania mwanzoni mwa mwaka ujao ikiwa ni juhudi za kuendeleza ushirikiano wa kimaendeleo kati ya benki hiyo na Tanzania.

Mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), inaendelea mjini Bali Indonesia ambapo imewakutanisha wadau wa masuala ya fedha wakiwemo Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi mbalimbali Dunia kujadili Sera na misaada inayotolewa na Taasisisi hizo.

Imetolewa na:-

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

                                                                                     Wizara ya Fedha na Mipango

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi