Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma amekagua hatua za ujenzi wa Kituo cha Michezo na Kupumzikia cha Dar es Salaam na kumwagiza mkandarasi wa mradi huo, Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) ya China kuongeza nguvu kazi ili kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Naibu Waziri Mwinjuma amesema hayo Agosti 19, 2023 alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa kituo hicho kinachojengwa kwenye eneo Changamani la Michezo lililopo karibu na Uwanja wa Benjamin Mkapa na Uhuru Temeke jijini Dar es Salaam.
“Nategemea tumepeana muda, nguvu kazi iongezeke ndani ya mwezi mmoja na nusu, itakapofika mwishoni mwa mwezi wa tisa, nitakuja tena kukagua. Tunataka huo muda wa mwezi mmoja uliopotea awe ameufidia na tumekubaliana kwenye jambo hilo”, amesema Naibu Waziri Mwinjuma.
Mhe. Mwinjuma amesema kuwa fedha ya Serikali awamu ya kwanza ya ujenzi huo imeshatoka, inapaswa kufanya kazi iliyokusudiwa na kuongeza kuwa michoro inaonesha kazi hiyo itakuwa na viwanja vya viwango vya sasa Duniani na Watanzania watanufaika na miundombinu hiyo.
“Mhe. Rais anataka kuona Watanzania wanapata miundombinu bora ya michezo, sisi tupo hapa kwa ajili ya kusimamia maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha hilo linatokea, chini ya uongozi wetu, tunataka viwanja kama tulivyokubaliana na vilivyoonekana kwenye mchoro”, amesema Naibu Waziri Mwinjuma.
Kituo hicho kitakuwa na viwanja vya michezo mbalimbali ikiwemo netiboli, mpira wa wavu, tenisi, viwili vya mpira wa miguu, vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo, jengo la utawala, bwawa la kuogelea lenye viwango vya kimataifa, sehemu ya michezo ya watoto, bwawa dogo la kuogelea, hostel pamoja na eneo la kuegesha magari.