Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Baraza la Vyama vya Siasa Laazimia Kumpongeza Rais Samia Kuboresha Mazingira ya Siasa
Aug 12, 2023
Baraza la Vyama vya Siasa Laazimia Kumpongeza Rais Samia Kuboresha Mazingira ya Siasa
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Mhe. Juma Ali Khatibu
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Mnamo Agosti 1, 2023, Baraza la Vyama vya Siasa chini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilifanya kikao maalum cha baraza hilo na kutoka na maazimio tisa ikiwemo azimio la kumpongeza na kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kuboresha mazingira ya kufanya shughuli za kisiasa nchini.

Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mhe. Juma Ali Khatibu ameyawasilisha Maazimio hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari.

Mwenyekiti, Mhe. Khatibu ameyataja maazimio mengine kuwa ni kundelea kutoa elimu kwa Vyama vya Siasa na umma kuhusu sheria zinazoratibu masuala ya vyama hivyo ili kuhimiza utawala wa sheria kwa madhumuni ya kudumisha amani, utulivu na umoja wa Taifa  pamoja na Vyama vya Siasa kuheshimu na kufuata sheria za nchi katika kutekeleza majukumu yao na viwajibishwe vinapokiuka sheria hizo.

“Tumeazimia kumpongeza na kumshukuru Rais, Mhe. Dkt. Samia kwa kuboresha mazingira ya kufanya shughuli za kisiasa nchini ikiwemo kuliwezesha Baraza la Vyama hivi kufanya kazi zake ipasavyo kwa kuongeza bajeti ya kuendesha shughuli za Baraza na Serikali yake kulipatia Baraza ushirikiano mkubwa", alieleza Mhe. Khatib.

Vievile, Baraza limeazimia  kuwa viongozi wa Vyama vya Siasa kujiepusha kutumia lugha za matusi, kibaguzi, udhalilishaji, upotoshaji na kubeza katika kutimiza malengo yao ya kisiasa badala yake kujikita kunadi sera zao kwa kujenga hoja na kutumia lugha yenye staha  na kujiepusha kuanzisha vikundi vya ulinzi vyenye mavazi na matendo yanayofanana na Majeshi ya Nchi kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria na kuhatarisha amani, utulivu na umoja wa kitaifa.

Aidha, Baraza hilo linashauri kuwa Taasisi za dini kujikita kutekeleza majukumu yao kadri va sheria za nchi na kujiepusha kutumia majukwaa ya kisiasa au nyumba za ibada kunadi sera za chama cha siasa, na Mamlaka za kiserikali zinazosimamia sheria mbalimbali za masuala ya kisiasa ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya  Siasa, Msajili wa Asasi za Kiraia, Tume ya Uchaguzi na Polisi ziendelee kusimamia sheria kwa umadhubuti ili kuweka mazingira ya amani, utulivu na umoja wa kitaifa.

Baraza pia, linashauri maboresho ya sheria ya Vyama vya Siasa na Uchaguzi yafanywe mapema iwezekanavyo ili kukabiliana na upungufu wa kisheria uliopo na changamoto zinazojitokeza katika kukuza demokrasia ya vyama vingi nchini.

Pia, Wizara inayohusika na suala la uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam iandae kikao na wajumbe wa Baraza la Vyama hivyo ili kuwapa fursa wajumbe wa Baraza uelewa kuhusu uwekezaji katika bandari hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi