Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Baraza la Mawaziri wa EAC Lapokea Mapendekezo ya Katibu Mkuu Mteule wa Jumuiya
Apr 16, 2024
Baraza la Mawaziri wa EAC Lapokea Mapendekezo ya Katibu Mkuu Mteule wa Jumuiya
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi wakifuatilia Mkutano wa 52 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki.
Na Mwandishi Wetu

Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) leo tarehe 16 Aprili, 2024 limepokea mapendekezo ya uteuzi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo katika kikao chake cha 52 cha Dharura kilichofanyika kwa njia ya mtandao.

 

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi.

 

Mapendekezo hayo yamewasilishwa kufuatia mabadiliko ya nafasi hiyo yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Samoei Ruto ambapo amemteua Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dkt. Peter Mutuku Mathuki kuwa Balozi wa Jamhuri ya Kenya nchini Urusi.

 

Hivyo, Mhe. Ruto amempendekeza Bi. Veronica Mueni Nduva kuchukua nafasi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya mara baada ya kuthibitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi wakijadili jambo wakati wa Mkutano wa 52 wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki

Katibu Mkuu wa Jumuiya huteuliwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kupokea mapendekezo kutoka kwa Mkuu wa Nchi husika kulingana na utaratibu wa mzunguko ambao unatoa kipindi cha miaka mitano ya kuhudumu katika nafasi hiyo.

 

Katibu Mkuu wa sasa, Dkt. Peter Mathuki aliteuliwa na Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 27 Februari, 2021. Hivyo, kulingana na muda wa kuhudumu Jamhuri ya Kenya imebakiwa na miaka miwili kukamilisha kipindi chake cha miaka matano (5).

 

Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri umeamua kuwa, katika kipindi cha mpito majukumu ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yatakaimiwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Forodha, Biashara na Fedha, Bi. Annette Ssemiwemba kulingana na kifungu 63 (3) cha Mkataba wa Uanzishawaji wa Jumuiyya hiyo.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi