Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Barabara ya Songwe – Vwawa Kukamilika Juni, 2022
Apr 11, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akijibu swali leo Bungeni jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema Serikali inaendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mahenje - Ndolezi - Hasamba hadi Vwawa ambayo ni muhimu kwa utalii na usafirishaji wa mazao mkoani Songwe.

Akijibu swali Bungeni leo lililoulizwa na Mbunge wa Vwawa Mhe. Japhet Hasunga, lililotaka kujua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo, Naibu Waziri Kasekenya amelihakikishia Bunge kwamba ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya kilometa 4.5 utakamilika ifikapo mwezi Juni, mwaka huu.

Aidha, amesema Serikali inaendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Igawa – Mbeya – Tunduma ili kupunguza msongamano wa magari katika barabara hiyo muhimu kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya ameliambia Bunge kuwa jukumu la usafi wa barabara na mifereji ikiwa ni pamoja na kuzibua makalavati ni la msimamizi wa barabara husika, hivyo kwa barabara Kuu na za Mikoa zinasimamiwa na TANROADS na barabara za Mijini na Vijijini zinasimamiwa na  TARURA.

Mhandisi Kasekenya alikuwa akijibu swali la Mhe. Naghejwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge Viti Maalum aliyetaka kujua ni nani hasa anayehusika na usafi wa mitaro pembeni mwa barabara.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi