Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bandari ya Uvuvi Kilwa Kuchochea Uwekezaji Viwanda vya Uchakataji Samaki
May 06, 2025
Bandari ya Uvuvi Kilwa Kuchochea Uwekezaji Viwanda vya Uchakataji Samaki
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza leo Mei 06, 2025 jijini Dodoma katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya sekta ya mifugo na uvuvi nchini katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa bandari ya uvuvi Kilwa Masoko itakapokamilika, itachochea uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya uvuvi.

Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza hayo jana Mei 6, 2025 katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma, wakati akieleza mafanikio na mwelekeo wa wizara hiyo ndani ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ameeleza kuwa, Serikali imeendelea na ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa Masoko kwa gharama ya shilingi bilioni 279.5 ambapo hadi kufikia Aprili, 2025, ujenzi huo umefikia asilimia 81.9 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2025.

“Pamoja na kuchochea ukuaji wa viwanda, bandari hiyo itawezesha meli za uvuvi zinazovua mazao ya uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania na Bahari Kuu kutia nanga na kushusha samaki wanaolengwa na wale wasiolengwa, pia meli hizo zitatia nanga kupata huduma mbalimbali za kijamii kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani ya nchi”, amesema Mhe. Ashatu.

Amefafanua kuwa, ujenzi huo umejumuisha: ujenzi wa gati lenye urefu wa mita za mraba 315; jengo la utawala; jengo la kuzalishia barafu, kuhifadhia, kuandalia samaki pamoja na soko la kuuzia samaki; kituo cha kusambazia maji safi; kituo cha zimamoto; kituo cha kupoozea umeme; kituo cha kuzalishia gesi ya naitrojeni; sehemu ya kuegesha magari; tanki za kuhifadhia mafuta; na karakana ya kutengenezea meli.

Vile vile, jumla ya wananchi 570 wamepata ajira ya moja kwa moja kupitia mradi huo.

Akizungumza kuhusu kufungua fursa za uchumi wa buluu, Mhe. Waziri amesema Serikali imeendelea kuliimarisha Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kwa kuliwezesha kufanya ukarabati wa gati kwa ajili ya kuegesha meli ambapo ukarabati huo unaendelea. Pia, imenunua gari tatu za ubaridi zenye uwezo wa kubeba uzito wa tani 10 kila moja na gari moja lenye uwezo wa kubeba tani tano kwa ajili ya kusafirisha mazao ya uvuvi.

Uwezeshaji huo, utaiwezesha TAFICO kufanya uvuvi wa Bahari Kuu na kufungua fursa zaidi katika uchumi wa buluu.

“Wizara itaendelea kuiimarisha TAFICO kwa kuwezesha ununuzi na usimikaji wa mtambo wa kuzalisha barafu tani 10, kukamilisha ununuzi wa meli mbili za uvuvi wa bahari kuu, kuanza ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mazao ya uvuvi na ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha chakula cha samaki kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo na Uvuvi ili kuwezesha Shirika hilo kuzifikia fursa za uchumi wa buluu na kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la taifa”, amemalizia Mhe. Dkt. Kijaji.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi