Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Balozi wa Uholanzi Nchini Mhe. Jeroen Verheul Atembelea JKCI
Jan 09, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_39650" align="aligncenter" width="1000"] Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Sulende Kubhoja akisalimiana na Balozi wa Uholanzi nchini Mhe. Jeroen Verheul wakati balozi huyo alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo wanazozitoa. Katikati ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Huduma ya Uuguzi Robert Mallya.[/caption]

Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepongezwa kwa jitihada zake inazozifanya  za  kuweza kuwafikia wananchi wengi  kwa  kutoa huduma bora za matibabu, elimu na ushauri wa jinsi ya kuepukana na magonjwa ya  moyo.

Pongezi hizo zimetolewa jana na Balozi wa Uholanzi nchini Mhe.  Jeroen Verheul  alipokuwa  akiongea na wafanyakazi wa Taasisi hiyo wakati wa ziara yake ya kuangalia huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa kwa wagonjwa.

 Mhe. Verheul alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ni moja ya Taasisi zinazofanya kazi vizuri ya kutoa huduma ya matibabu ya moyo  katika nchi zilizopo Kusini mwa Afrika .

[caption id="attachment_39651" align="aligncenter" width="1000"] Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Huduma ya Uuguzi Robert Mallya akiongea jambo na Balozi wa Uholanzi nchini Mhe. Jeroen Verheul wakati balozi huyo alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo wanazozitoa. Kushoto ni Mhandisi wa umeme wa Taasisi hiyo Victor Kaduma.[/caption]

Kuhusu Ubalozi wake  kushirikiana na Taasisi hiyo katika utoaji wa huduma kwa wananchi alisema ataangalia ni jinsi gani watashirikiana  katika programu  mbalimbali za afya ambazo zinatolewa  hapa nchini kupitia  Ubalozi wa Uholanzi.

“Wiki tatu zijazo nitaenda nchini Uholanzi ambako tuna mkutano wa mabalozi wote. Kupitia mkutano huo nitaangalia ni Taasisi ipi ambayo itaweza kuja nchini kufanya matibabu ya moyo kama ilivyokuwa kwa nchi zingine ambazo zinatuma wataalamu wake kuja  katika Taasisi hii kutoa huduma za matibabu kwa wananchi”,alisisitiza Mhe. Verheul.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi alimshukuru Mhe. Balozi kwa kuwatembelea na kuona huduma mbalimbali wanazozitoa  na kusema kuwa wanajitahidi kuhakikisha kila mwananchi anayefika katika Taasisi hiyo anapata huduma bora za matibabu ya moyo.

[caption id="attachment_39652" align="aligncenter" width="1000"] Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimweleza Balozi wa Uholanzi nchini Mhe. Jeroen Verheul jinsi maendeleo ya ukarabati wa wodi ya watoto unavyoendelea wakati balozi huyo alipotembelea JKCI kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo wanazozitoa. Ukarabati wa jengo hilo ukikamilika litakuwa na vitanda 32 na vitanda tisa katika chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU).[/caption] [caption id="attachment_39653" align="aligncenter" width="1000"] Balozi wa Uholanzi nchIni Mhe. Jeroen Verheul akiwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kusubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo. Mhe. Verheul alitembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moto wanazozitoa kwa wananchi.[/caption]

Alisema idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka ukilinganisha na miaka ya nyuma hii inaonyesha kuwa hivi sasa wananchi wenye matatizo ya moyo wanaelewa ni wapi pa kwenda kutibiwa magonjwa hayo.

“Kutokana na wataalamu wetu kuwa na utaalamu wa kutosha na hospitali kuwa na vifaa vya kisasa tumeweza kufanya upasuaji kwa wagonjwa wengi zaidi kwa mwaka 2018 ukilinganisha na mwaka 2017”.

“Mwaka 2018 tumefanya upasuaji wa kufungua kifua kwa wagonjwa 1053 na bila kufungua kifua kwa wagonjwa 405 ambapo mwaka 2017 tulifanya upasuaji wa kufungua kifua kwa wagonjwa 225 na bila kufungua kifua kwa wagonjwa 800”, alisema Prof. Janabi.

Akiwa katika Taasisi hiyo Mhe. Balozi Verheul alitembelea maabara ya uchunguzi wa matatizo na tiba za magonjwa ya moyo (Cath Lab), jengo jipya la watoto ambalo ukarabati wake ukikamilika   litakuwa na vitanda  32 na vitanda tisa katika  chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU), wodi ya watoto na wagonjwa waliofanyiwa na wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua,  chumba cha upasuaji na chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU).

[caption id="attachment_39654" align="aligncenter" width="1000"] Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi na Balozi wa Uholanzi nchini Mhe. Jeroen Verheul pamoja na wafanyakazi wa Taasisi hiyo wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kwa ziara ya Mhe. Balozi ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa kwa wananchi.[/caption] [caption id="attachment_39655" align="aligncenter" width="1000"] Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiagana na Balozi wa Uholanzi nchini Mhe. Jeroen Verheul mara baada ya balozi huyo kumaliza ziara yake ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi hiyo kwa wananchi.[/caption]

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi