Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Balozi Mwadini ateta na Wataalam wa Wizara Kufanikisha Kongamano la Kiswahili Ufaransa
Feb 15, 2026
Balozi Mwadini ateta na Wataalam wa Wizara Kufanikisha Kongamano la Kiswahili Ufaransa
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa Mhe. Jabir Mwadini, akifanya kikao na wataalamu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na wadau wa Sekta kuhusu maandalizi ya Kongamano la Kiswahili la Kimataifa linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 27-30 Aprili 2026 Jijini Paris, Ufaransa.
Na Mwandishi Wetu

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa Mhe. Jabir Mwadini,  amefanya kikao na wataalamu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  pamoja na wadau wa Sekta kuhusu maandalizi ya Kongamano la Kiswahili la Kimataifa linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 27-30 Aprili 2026 Jijini Paris, Ufaransa.

Katika kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Mhe. Mwadini amehimiza umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi na Diaspora katika kuhakikisha  kongamano hilo linafanikiwa vizuri na kufikiwa kwa malengo ya kuanzishwa kwake ikiwamo, kuitangaza Tanzania kimataifa na kuimarisha diplomasia ya kiuchumi. Akisistiza kuwa, Ubalozi uko tayari kutoa ushirikiano stahiki kuelekea kongamano hilo.

Kwa upande wake, Bw. Boniface Kadili Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni alimshukuru Mhe. Balozi kwa kuendelea kushirikiana na Wizara na Taasisi mbalimbali katika kuhakikisha kuwa, maandalizi ya kongamano hilo yanafanyika vizuri na kuleta tija. Lengo ni kukuza na kuendeleza lugha adhimu na aushi ya Kiswahili kimataifa na kuchochea maendeleo ya sekta za utalii, elimu, biashara na uwekezaji.

Aidha, Bw. Kadili aliupongeza Ubalozi huo kwa jitihada za kukipenyeza Kiswahili katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambapo kwa sasa Kiswahili ni moja ya lugha rasmi ya Mikutano Mikuu ya shirika hilo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi