Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Balozi Mulamula Ataja Maeneo 11 ya Kujivunia Mambo ya Nje
Mar 15, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Georgina Misama – MAELEZO, Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ametaja maeneo 11 ambayo Wizara yake inajivunia kuelekea mwaka Mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita madarakani.

Akizungumza leo katika mkutano na waandishi wa habari uliohusu mafanikio ya serikali ya awamu ya Sita madarakani Balozi Mulamula alisema tangu serikali ya awamu ya Sita kuingia madarakani, Wizara imetekeleza majukumu yake kwa mafanikio ambapo miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho ni kuongezeka kwa ziara za viongozi ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja viongozi Wakuu wa kitaifa walifanya ziara nje ya nchi na viongozi wakuu kutoka nchi mbalimbali na Mashirika ya Kimataifa walitembelea hapa nchini.

Kupitia ziara hizo za viongozi wakuu zimeimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali na mashirika ya Kimataifa na Kikanda, kadhalika kupitia ziara hizo Tanzania imenufaika na kusainiwa kwa makubaliano na mikataba ya ushirikiano katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa”, alisema Balozi Mulamula.

Aidha, upatikanaji wa misaada na mikopo ya masharti nafuu ambapo fedha kiasi cha Shilingi Trilioni 1.77 na Euro milioni 425 kutoka Kamisheni ya Umoja wa Ulaya zilipatikana, wakati huohuo Tanzania ilichaguliwa na nchi 192 wanachama wa Umoja wa Mataifa kuwa Makamu wa Rais wa Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo katika uchaguzi huo, Tanzania ilipita bila kupingwa, mara ya mwisho Tanzania kupata nafasi hiyo ilikuwa mwaka 1991.

Tanzania imefungua Balozi mpya mbili (2) katika nchi za Austria na Indonesia na Konseli Kuu tatu (3) katika miji ya Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Shanghai na Guangzhou nchini China, ujenzi na ukarabati wa majengo balozini pamoja na utafutaji wa masoko ya bidhaa za Tanzania.

Maeneo mengine yaliyofanya vizuri ni uwekezaji kutoka nje ambapo Wawekezaji wengi wameonesha dhamira ya kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali na baadhi yao wameanza taratibu za uwekezaji lakini pia Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa Kituo cha SADC cha Uratibu wa Kupambana na Ugaidi kilichozinduliwa Jijini Dar es Salaam tarehe 28 Februari, 2022.

Balozi Mulamula alisema Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine imeendelea na mikakati yake ya kuhamasisha kukuza na kusambaza matumizi ya lugha ya Kiswahili duniani, "Mikakati hiyo imetoa matokeo chanya ambapo kwa mara ya kwanza kiswahili kimetambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na kuwekewa siku maalum ya kuadhimishwa duniani ambayo ni tarehe 7 Julai kila mwaka. Niwakumbushe kuwa, Kiswahili ni lugha ya kwanza ya kiafrika kupewa hadhi hiyo na UNESCO”, alisisitiza.

Vile vile wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru yaliyofanyika mwezi Desemba 2021, Balozi za Tanzania zilisheherekea kwa ubunifu wa hali ya juu, ambapo Balozi zote zilijipanga kutumia maadhimisho hayo kwa kuandaa makongamano, maonesho, mikutano na shughuli mbalimbali kwa ajili ya kutangaza fursa zilizopo nchini hususani biashara, uwekezaji, utalii na bidhaa za Tanzania katika maeneo yao uwakilishi.

Balozi Mulamula alihitimisha na Suala la Watanzania waliokuwepo Ukraine ambapo alisema serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha raia wake wanakuwa salama pamoja na changamoto hizo.

Napenda kuwafahamisha kuwa, zoezi la kuwaondoa Watanzania wote waliokuwepo nchini humo wakiwemo Wanafunzi limekamilika ambapo hadi sasa takribani Watanzania 300 wamefanikiwa kuondoka na kuelekea nchi jirani na baadhi yao wamerejea hapa nchini ”, alisema.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi