Na Mwandishi wetu, Dar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Czech, Bw. Roman Grolig katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wamekubaliana kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Jamhuri ya Czech katika sekta za biashara na uwekezaji, kilimo, elimu na teknolojia.
Balozi Mulamula aliwakaribisha wawekezaji kutoka Czech kuwekeza nchini pamoja na kutia mkazo wa kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na Czech.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Czech, Bw. Grolig amesema ataendelea kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Czech kuja kuwekeza Tanzania kwani ni sehemu salama ya kuwekeza.
“Jamhuri ya Czech imedhamiria kuongeza ushirikiano na Tanzania na katika kutimiza azma hiyo, wafanyabiashara na wawekezaji wameonesha nia ya kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza ndege ndogondogo pamoja na magari makubwa hapa Tanzania,” amesema Bw. Grolig
Pia ameongeza kuwa kwa sasa Czech ipo katika mchakato wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja hapa nchini Tanzania ili kuwawezesha wawekezaji na wafanyabiashara kusafiri kwa urahisi kuja Tanzania kutafuta fursa za uwekezaji,” amesema Bw. Grolig.