Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Balozi, Mhandisi Aisha Amour ametoa wiki moja kwa mkandarasi SINOHYDRO CORPORATION LTD anayejenga Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Msalato, Mshauri Mwelekezi M/S BEZA na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, kutayarisha mkakati utakaowezesha kukamilika kwa ujenzi wa kiwanja hicho kabla ya Disemba 2024.
Balozi Amour, ameyasema hayo baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanja hicho na kuelezea kutoridhishwa kwake na kasi ya ujenzi inayoendelea.
“Kwa kweli sijaridhishwa na kasi yenu, nataka mnipe mkakati utakaowezesha kiwanja hicho kukamilika kwa wakati na kwa viwango”, amesesitiza Balozi, Mhandisi Amour.
Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Msalato awamu ya kwanza unahusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege (runway), barabara za maungio (Taxi way), maegesho ya ndege (apron), uzio wa usalama, barabara ya kuingia na kutoka kiwanja cha ndege (access roads), maegesho ya magari (car parking) na usimikaji wa mfumo wa taa za kuongozea ndege (AGL ) ambao hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 30.91 wakati awamu ya pili ya ujenzi huo ikihusisha ujenzi wa jengo la abiria na miundombinu yake.
Katika hatua nyingine Balozi, Mhandisi Amour amekagua ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa Dodoma (Dodoma Outer ring road) ambayo ina sehemu mbili, Nala- Veyula-Mtumba –Ihumwa dry port Km 52.3 na sehemu ya pili Ihumwa -Matumbulu –Nala Km 60 na kuwataka wakandarasi wanaojenga barabara hizo kuja na mikakati itakayowezesha kwenda kwa kasi kabla ya mvua za Elnino kuanza.
“Tusingependa visingizio vya mvua kwa sababu Mamlaka ya Hali ya Hewa imeshatuonya kutakuwa na mvua nyingi, ni vizuri kazi zinazotakiwa kufanyika sasa zikafanyika mapema ili kuepuka usumbufu”, amesisitiza Mhandisi Amour.
Kwa upande wake Mkandarasi wa China Civil Construction Corporation anayejenga sehemu ya kwanza Nala- Veyula-Mtumba –Ihumwa dry port Km52.3 na Beijing Economic and Technology Development anayejenga sehemu ya pili ya Ihumwa -Matumbulu –Nala Km 60 wameahidi kutekeleza maelekezo hayo ili kukamilisha ujenzi huo kwa mujibu wa mkataba na katika ubora stahiki.