Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Bajeti Kuu ya mwaka 2022/23, imejipanga kuongeza kasi ya kufufua Uchumi na kuimarisha Sekta za Uzalishaji kwa ajili ya Kuboresha Maisha.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Bajeti Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2022/23.
Dkt. Nchemba amesema kuwa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/23 ni ya pili katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 - 2025/26 wenye dhima ya kujenga Uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.
“Aidha, dhima kuu ya bajeti ya mwaka 2022/23 kama ilivyokubaliwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni “Kuongeza Kasi ya Kufufua Uchumi na Kuimarisha Sekta za Uzalishaji kwa ajili ya Kuboresha Maisha”. Alisema Dkt. Mwigulu.
Waziri Dkt. Mwigulu ameongeza kuwa, katika utekelezaji wa dhima hiyo kwa mwaka 2022/23, kipaumbele kitakuwa katika sekta za uzalishaji zikiwemo Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Nishati, Uwekezaji na Biashara kwani lengo la Serikali ni kujenga uchumi, kukabiliana na umasikini pamoja na ukosefu wa ajira hasa kwa vijana.
Vilevile, Mhe. Dkt. Mwigulu amezitaja shabaha za uchumi jumla katika kipindi cha
mwaka 2022/23 kuwa ni ukuaji wa Pato halisi la Taifa kufikia asilimia 4.7 mwaka 2022 na asilimia 5.3
kwa mwaka 2023 pia, kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa
bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja.
Shabaha zingine ni Mapato ya ndani kufikia asilimia 14.9 ya Pato la Taifa mwaka 2022/23, Mapato ya kodi kufikia asilimia 11.7 ya Pato la Taifa mwaka 2022/23 na kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.