Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Awamu ya Tano Yafanya Mageuzi Makubwa Sekta ya Madini
Jun 17, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_53283" align="aligncenter" width="768"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipeana mkono na Rais wa kampuni ya Barrick Dkt. Mark Bristow katika hafla ya utiaji saini wa mikataba ya makubaliano ya kuendesha kwa pamoja kapuni ya Twiga ya uchimbaji wa Madini kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick ambapo kwa sasa kampuni mpya ya ubia ya Twiga, Serikali itakuwa na hisa ya asilimia 16 .Halfa iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam. Januari 24, 2020.(Picha kutoka Maktaba)

[/caption]

Jonas Kamaleki, Dodoma

Mageuzi makubwa yamefanyika katika Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na kuanzisha Wizara mahsusi ya Madini, kudhibiti utoroshaji na usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi, kuanzisha masoko ya madini kwenye kila Mkoa, kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara wetu wadogo kwenye mnyororo wa uchumi wa madini na kuwafutia ama kuwapunguzia viwango vya kodi.

Kauli hiyo ilitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akihutubia Bunge na kulivunja jana jijini Dodoma.

“Mwezi Julai 2017, tulipitisha Sheria ya Kulinda Rasilimali za Taifa (The Natural Wealth and Resources – Permanent Sovereignty - Act 2017), ikiwemo madini, nakushukuru sana wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kupitisha Sheria hii muhimu sana kwa Taifa letu. Kwa hakika, mmeingia kwenye vitabu vya historia vya nchi yetu na naamini vizazi hadi vizazi vitawakumbuka”, alisisitiza Rais Magufuli.

Aidha,  Rais Magufuli alisema kuwa kupitishwa kwa Sheria hiyo ndiko kumewezesha kwa mara ya kwanza Watanzania kumiliki rasilimali zao kwa nguvu za kisheria. Na Sheria hiyo pia ndiyo imefanikisha kuanzishwa kwa Kampuni ya Twiga Minerals Company, ambayo Serikali inamiliki hisa asilimia 16 na Kampuni ya Barrick asilimia 84 ya Hisa, na halikadhalika kutolewa kwa malipo ya fidia ya Dola za Marekani milioni 100 kati ya Dola za Marekani 300 ambazo Kampuni ya Barrick ilikubali kutulipa kufuatia majadiliano yaliyofanyika.

Rais Magufuli alimshukuru Spika kwa kuunda Kamati Maalum ya Bunge ya Kuchunguza Utoroshaji wa Madini ya Tanzanite, ambayo ilitoa ushauri wa kujenga Ukuta wa kilometa 25 katika Mgodi wa Mirerani, ambao Serikali iliutekeleza.

Kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali, sekta ya madini sasa imeanza kukua kwa kasi kubwa, ambapo mwaka jana (2019) iliongoza kwa ukuaji (kwa asilimia 17.7), ikifuatiwa na ujenzi asilimia 14.1.

Aidha, mapato yatokanayo na madini nayo yameongezeka. Mathalan, kwenye mwaka wa Fedha 2018/2019 zilikusanywa shilingi bilioni 346 kutoka shilingi bilioni 194 mwaka 2016/2017.

“Kwenye Mwaka huu wa Fedha (2019/2020) tunatarajia tukusanye shilingi bilioni 470, ambapo mwezi Aprili 2020 pekee, licha ya kuwepo kwa tatizo la ugonjwa wa corona, tumekusanya shilingi bilioni 58. Haijawahi kutokea. Kiwango cha juu kabisa tulichowahi kukikusanya kwa mwezi ilikuwa shilingi bilioni 43”, alisisitiza Rais Magufuli.

Mafanikio mengine yaliyopatikana kwenye sekta ya madini ni kutolewa kwa leseni 221 za uchenjuaji madini, leseni 4 za uyeyushaji madini (smelting) na leseni 4 za usafishaji madini (refining). Vilevile, Serikali imetenga hekta 38,567 kwa ajili ya uchimbaji mdogo na kuwapatia mafunzo wachimbaji wadogo 10,338. Kwa mujibu wa Rais Magufuli hivi sasa wachimbaji wadogo hawabughudhiwi.

Zamani wachimbaji wadogo waliendesha shughuli zao kama wakimbizi, Serikali ilifanya juhudi za makusudi kuhakikisha wananchi hawabughudhiwi wala kufawafanya kuwa wakimbizi ndani ya Taifa lao.

Tanzania imejaliwa kuwa na karibu madini yote yanayopatikana duniani ikiwemo Tanzanite inayopatikana nchini peke yake. Madini hayo kwa muktadha huu yataifanya nchi hii kujitegemea kibajeti na kuchangia sehemu kubwa ya  maendeleo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi