Na: Jonas Kamaleki
Mkazi wa Mkoa wa Iringa, Thomas Lubinza ametembea zaidi ya kilometa 502 kutoka Iringa mpaka Dar es Salaam kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zote anazozifanya katika kulinda na kusimamia raslimali za watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari, Lubinza amasema kuwa Rais Magufuli kwa kipindi kifupi cha uongozi wake ameweza kufanya mambo makubwa ikiwemo kudhibiti na kupambana na vitendo vya rushwa, kurudisha nidhamu serikalini na kuboresha miundombinu.
Licha ya juhudi hizi zinazofanywa na Mhe. Magufuli,wapo ambao wanabeza jitihada hizi na wengine kukejeli, alisema Lubinza na kuongeza kuwa yeye ameona ni vyema ajitokeze kumpongeza.
“Tunafahamu fika kuwa lengo la watu wengine ni kumvunja moyo Mheshimiwa Rais ili aachane na vita hiyo ya kupambana na maovu, mimi pamoja na watanzania wengine wenye nia njema na nchi hii bila ya kujali tofauti zetu za kisiasa, kikabila, kidini hata kikanda tumeamua kuunga mkono waziwazi kwa hatua zinazochukuliwa na Serikali yetu”, alisisitiza Lubinza.
Aidha, Lubinza amewaomba watanzania wote wamuunge mkono Mhe. Rais Magufuli kwani nia yake ni njema ya kuibadilisha Tanzania na kuifanya nchi yenye uchumi mzuri wa viwanda.
Ameongeza kuwa ameamua kufanya matembezi ya hiari ili kujionea kero za wananchi wakati akiwa njiani kuelekea Dar es Salaam. Ametaja baadhi ye kero hizo kuwa ni ukosefu wa maji, masoko ya kuuzia mazao ya wakulima, na madereva kutokuwa na mikataba mizuri.
Lubinza amesema licha ya changamoto hizo, Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi kutatua changamoto nyingi hapa nchini ikiwemo migogoro ya ardhi, kuboresha elimu na kuitoa bure, kuimarisha sekta ya afya na kuboresha usafiri na usafirishaji.
Safari hii alianza Juni 17, 2017 akitokea Iringa mjini kuelekea jijini Dar es Salaam, ambapo aliwasili Juni 26 ikiwa ni takriban siku tisa.
Rais John Pombe Magufuli ameungwa mkono na makundi ya watu mbali mbali ndani na nje ya nchi. Uungwaji mkono huu umeshika kasi hasa baada ya kuzuia mchanga wa madini kusafirishwa nje ya nchi na kuunda tume mbili kuchunguza aina na thamani ya madini yanayopatikana katika mchanga huo. Tume hizo zikiongozwa na maprofesa zilitoa matokeo ambayo yaliwasimumua watanzania na watu wengine nje ya nchi.
Ameungwa mkono na wasomi wa vyuo vikuu, vijana wazalendo, viongozi wa dini na na wananchi wa kawaida. Hakika juhudi zake Rais Magufuli kurekebisha Taifa zimekuwa dhahiri.