Na Tiganya Vincent - RS Tabora
Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Magharibi Tabora, Isaac Laise amesema Watanzania wanatakiwa kutoruhusu mataifa ya nje yawagawanye kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
Alisema kuna baadhi ya mataifa makubwa yanaweza kutaka kupenyeza ajenda zao ili kujinufaisha kisiasa au kiuchumi na kuiacha Tanzania ikiwa imegawanyika kama wananchi hawatakuwa makini kulinda umoja wao.
Askofu Laise alisema hayo hivi karibuni mjini Tabora wakati akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kongamano la ulinzi na usalama lilioandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora na kuwashilikisha wadau mbalimbali.
Alisema Watanzania wanapaswa kuwa waangalifu na mataifa makubwa ambayo yanakuwa na ajenda zao binafisi na zinaposhindwa kufanikiwa wanaweza kuwagawanya kwa misingi ya udini, ukabila hata itikadi ya kisiasa ili kuhakikisha wanachohitaji wanakipata.
“Tusiruhusu maadui wa nje watugawanye kwa ajili ya maslahi yao ya kisiasa au kiuchumi ambayo wakati mwingine yako kwa ajili ya kutaka kunyonya rasilimali hapo nchini , jambo la msingi ni kuendelea kulinda umoja wetu, amani na utulivu tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu” alisema Askofu huyo.
Alisema kila Mtanzania anapaswa kuwa mdau mkubwa wa amani ya nchi hii kwa kuilinda na kuitunza ili hatimaye iweze kumsaidia katika shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo yake na Taifa kwa ujumla.
Aidha Askofu Laise alisema kila mwananchi katika nafasi yake ni lazima atende haki na kusiwepo na vitendo ambavyo vinalazimisha haki kununuliwa
Alisema katika nyakati hizo ambapo Serikali inapambana na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijinufaisha na rasilimali za taifa kwa maslahi yao kutumiwa na mataifa makubwa kuwagawanya kwa misingi ya udini, ukabila hata itikadi za kisiasa.