Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Asilimia 71 ya Wasichana Ruvuma Wapatiwa Chanjo ya Kuzuia Saratani ya Mlango wa Kizazi
Apr 30, 2019
Na Msemaji Mkuu

Revocatus Kasimba - Songea

Mkoa wa Ruvuma umefanikiwa kutoa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 kwa asilimia 71 ya lengo kwa mwaka 2018

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema  kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma alisema chanjo hiyo ilianza kutolewa mwezi Aprili mwaka 2018 katika Halmashauri nane za mkoa wa Ruvuma.

Alitoa taarifa hiyo jana mjini Songea wakati wa kikao cha kamati ya Afya ya Msingi mkoa kutathamini zoezi la utoaji chanjo hii kwa viongozi wa mkoa na halmashauri zote

Pololet alisema lengo la chanjo hiyo ni kuwakinga mabinti dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi ambayo inaongoza kwa  vifo vya akina mama nchini.

“Wasichana umri wa miaka 14 waliochanjwa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi mkoa wa Ruvuma ni 14,786 sawa na asilimia 71 ya lengo la kuchanja wasichana 16,631 sawa na asilimia 80,” alisema Pololet.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt.Jairy Khanga alisema changamoto zilizojitokeza  wakati wa zoezi hata mkoa kushindwa kufikia lengo la asilimia 80 ni pamoja na imani potofu kwenye baadhi ya maeneo kuwa chanjo hii inaweza kuzuia mabinti kuzaa

Ametaja halmashauri za Tunduru,Namtumbo na Madaba kufanya vibaya kwenye utoaji wa chanjo hii kutokana na viashiria vya  uwepo wa imani potofu kwenye jamii hivyo wasichana kutojitokeza kupata chanjo

Dkt.Khanga alizitaja halmashauri zilizofanya vizuri mwaka huu kuwa ni Mbinga DC (100%) na Nyasa (83%)

“Serikali imeridhia chanjo hii kutolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 baada ya kufanya utafiti kujiridhisha kutokuwa na madhara kwa watu “ alisema Dkt.Khanga

Dkt.Khanga alitoa wito kwa viongozi wa dini na mila kwenye mkoa wa Ruvuma kusaidia kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo hii kwani Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha ubora wake katika kudhibiti saratani ya mlango wa kizazi.

Kwa mujibu wa Dkt Khanga , vifo 403,000 vilitokea nchini Tanzania kwa mwaka kutokana na saratani ambapo saratani ya mlango wa kizazi kwa akinamama iliachangia asimilia 37.

“Saratani ya shingo ya uzazi Tanzania inaathiri zaidi ya (37%),saratani ya matiti (12%) na saratani ya koo (6.7%) ndio maana serikali ikaja na mkakati wa kuzuia isiendelee “ alisisitiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Katika kikao hicho cha tathmini mkoa uliazimia kuhakikisha unafanya ufuatiliaji wa mabinti waliokwisha chanjwa kujua maendeleo yao na kuhuisha taarifa za halmashauri.

Wito umetolewa pia kwa viongozi wa wilaya kuendelea kuhamasisha wananchi kuhusiana na chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kupitia vyombo vya habari na sanaa katika maeneo yao

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi