Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Asilimia 53 ya Watanzania Wasema Usalama Umeimarika Nchini- Twaweza
Jul 27, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Agness Moshi na Jonas Kamaleki 

Zaidi ya nusu ya Watanzania wamesema kuwa hali ya usalama nchini imeimarika  ikilinganishwa na miaka takriban miwili iliyopita na kuwafanya wananchi waishi kwa utulivu na amani.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la Kiserikali lijulikanalo kama Twaweza, Bw. Aidan Eyakuze wakati akiwasilisha matokeo utafiti wa “Hapa Usalama Tu: Usalama, Polisi na Haki nchini Tanzania” kupitia sauti za wananchi kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.

Bw. Eyakuze alisema kuwa takwimu zilizo kusanywa na sauti za wananchi kwa mwaka huu zimeonesha kuimarika kwa usalama kwa wananchi wa Tanzania Bara ikilinganishwa na miaka iliyopita.

“Tumeongea na watu 1805 kuwauliza hali ya usalama katika maeneo wanayoishi na asilimia 53 ambayo ni sawa na nusu ya Watanzania Bara wamesema hali ya usalama imeimarika na inaridhisha” alisema Bw.Eyakuze.

Bw.Eyakuze amesisitiza kuwa wamekusanya taarifa kutoka kwa wananchi wenyewe,  kupitia simu zao za mikononi ambapo wameona kuwa watanzania wengi wapo kwenye hali ya usalama na hii inamewapa taswira tofauti na taarifa zinazotolewa na vyombo  vya habari.

Aidha, Bw.Eyakuze amesema kuwa asilimia 47 ya wananchi wanaridhishwa na utendaji kazi wa jeshi la Polisi nchini kutokana na kuzuia na kutatua uhalifu na kuwajali wananchi.

Ripoti hiyo imeonyesha kuwa wananchi wanapata pia ulinzi kutoka kwa polisi jamii, maarufu kama sungusungu na asilimia 41 ya wananchi wamesema wana vikundi vya sungusungu katika maeneo yao na wanaridhika na huduma zinazotolewa.

Utafiti huu ulifanyika mnamo Aprili 2017 ukihusisha mikoa yote ya Tanzania Bara na wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumuia simu za mkononi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi