Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ahadi Yetu ni Kujenga Miradi ya Maji Nchi Nzima - Rais Samia
Jun 06, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Grace Semfuko, MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maji nchi nzima ili kuwahakikishia Watanzania huduma bora ya maji safi na salama kama ilivyoahidi wakati inaingia madarakani.

Amesema lengo la Serikali ni kuwa, ifikapo mwaka 2025, huduma ya maji safi na salama inafikia asilimia 85% kwa Vijijini na asilimia 95% Mijini ambapo mpaka sasa miradi hiyo inaendelea kujengwa na imefikia hatua nzuri.

Ameyasema hayo leo Juni 06, 2022 Jijini Dodoma, wakati akishuhudia utiaji saini makubaliano ya mikataba ya ujenzi wa miradi ya maji katika miji 28, yenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 500 ambayo inatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mkopo wenye masharti nafuu, kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim.

"Serikali itaendelea kujenga miradi ya maji katika kila eneo kwenye nchi yetu, ili kuhakikisha tunatimiza ahadi yetu kwamba ifikapo mwaka 2025, huduma ya maji safi na salama inafikia asilimia 85% Vijijini na asilimia 95% Mijini, kuna dalili zote kwamba tutaweza kwa sababu mpaka sasa, kwa Vijijini tumeshafanya asilimia 74% lakini miradi 1,000 inayoendelea vijijini itakuja kuchangia asilimia 4%, kwa hiyo mpaka juni mwakani tutakuwa tumefikia asilimia 78%, tuna miaka mingine miwili ya utekelezaji ambayo itatusogeza, lakini kwa upande wa miji tupo 89.9% kwa hiyo mpaka muda huo tutafika na kupita ile ahadi yetu” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais ameipongeza Wizara ya maji kwa kufanya vizuri katika kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maji nchi nzima na kuongeza kuwa lengo la Serikali la kuhakikisha huduma hiyo inapatikana nchini linatimia ifikapo mwaka 2025.

"Ni ukweli kwamba Wizara ya maji imebadilika sana, nawashukuru sana, mlinipa tabu mwanzo, tumeelezana ukweli mambo ya kubuni miradi mikubwa kuliko inayotakiwa lakini temeelezana ukweli mpo kwenye mstari, sasa tunakwenda vizuri, mradi huu badala ya miji 16 tumekwenda mpaka miji 28, kuna maeneo yalihitaji mabomba 6 tu lakini kwenye design kuna mabomba 21, sasa vile mmerudi mmekaa vizuri, mradi huu unakwenda kuwanufaisha watu, hata kwa miradi hii tunayosaini leo mmejitahidi sana kubana matumizi”, amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amesema tangu kuingia madarakani kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na mabadiliko makubwa katika sekta ya maji ambapo zamani wizara hiyo iliitwa wizara ya Ukame na sasa jina limebadilika.

"Mheshimiwa Rais tunakushukuru kwa sababu wizara yetu umeibadili, imetoka kuwa Wizara ya lawama, Wizara ya kero, sasa hivi imekuwa wizara ya utatuzi na matumaini kwa Watanzania, umeitoa wizara hii kuwa wizara ya ukame leo hii ni wizara ya maji, sisi viongozi wa wizara ya maji tutafia saiti, hatutacheka na Wakandarasi wanaotukwamisha, tutacheka na maji tu, Wizara yetu ya maji miaka ya nyuma utekelezaji wake haukuwa wa kuridhisha, ukaamua kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), tulikuwa na miradi 177 kichefuchefu ambayo haikuwa ikitoa maji, ndani ya mwaka mmoja tumeshakwamua miradi 126 kupitia RUWASA, katika mwaka huu wa fedha tunakwenda kutekeleza miradi 1,029, hii haijawahi kutokea” amesema Waziri Aweso.

Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa, amesema fedha hizo zimeisaidia Wizara yake kuongeza nguvu katika kuwapatia huduma za maji safi na salama Watanzania wengi zaidi na kuvuka malengo ya wizara.

"Mheshimiwa Rais, fedha hizi Shilingi trilioni 1.73 ambayo umetusaidia kwenda kuwatua akina mama ndoo kichwani ni fedha nyingi sana, upande wa Serikali za Mitaa kwenye bajeti ya mwaka 2022/23 ambayo umetupitishia, Serikali za mitaa tumepanga kukusanya shilingi Trilioni 1.01, sasa ukichukua makusanyo ya Halmashauri zote 184 nchini, kwa mwaka mzima ni sawa na fedha hizi ambazo leo hii tunashuhudia zinaenda kwenye miji 28” amesema Mhe. Bashungwa.

Nae Balozi wa India Nchini Tanzania Bw. Binaya Srikanta Pradhan amesema nchi yake inaendelea kushirikiana na Tanzania, katika kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama ambapo mpaka sasa Serikali ya nchi yake, imetoa zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 1 katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji nchini Tanzania.

“Mheshimiwa Rais, kusaini kwa mkataba huu wa Dola za Marekani shulingi Milioni 500 leo hii, unaongeza nia yetu katika kuongeza kutekeleza miradi ya maji ambayo sasa inafikia Dola za kimarekani zaidi ya Bilioni 1, na miradi hii itanufaisha zaidi ya watu milioni 6.12, nikuhakikishie kwamba miradi hii tunayoisaini leo itatekelezwa katika mafungu manne, nakuahidi kwamba mimi mwenyewe nitasimamia miradi hii ili itekelezwe katika ubora unaotakiwa, katika uongozi wako kumekuwa na mageuzi makubwa yanayosifiwa kimataifa, India itaendeleza ushiriki wake katika Serikali ya Tanzania” amesema Balozi Binaya.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi