Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Agizo la Rais Magufuli la Kujengwa Kiwanda cha Kuchakata Samaki Mkoani Rukwa Latekelezwa
Aug 17, 2020
Na Msemaji Mkuu

Mkurugenzi Mtendaji, Alpha Tanganyika Flavour, Alpha Nondo (kulia aliyenyoosha mkono) akimuonesha Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (aliyekaa) namna kiwanda cha Alpha cha kuchakata samaki kitavyokuwa kinaonekana baada ya kukamilika kwa ukarabati wake alipotembelea kukagua ukarabati unaoendelea wa kiwanda hicho kilichopo mkoani Rukwa leo Agosti 13, 2020. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi (WMUV), Stephen Lukanga.

Na Mbaraka Kambona, Rukwa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alipofanya ziara mkoani Rukwa mwaka jana, moja ya maelekezo yake kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha kuwa katika Mkoa huo kunaanzishwa kiwanda cha kuchakata samaki ili kuwasaidia wavuvi wa maeneo hayo kupata soko la uhakika kwa samaki wao.

Kufuatia agizo hilo, Kampuni ya Alpha Tanganyika Flavour kupitia ushirikiano mkubwa kutoka kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wameweza kufanya uwekezaji katika sekta hiyo ya uvuvi kwa kuanzisha kiwanda cha kuchakata samaki ambacho kwa sasa kinamalizia ukarabati wake kabla ya kuanza kazi mwishoni mwa mwezi wa tisa, mwaka huu.

Hayo yalifahamika, baada ya Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah alipofanya ziara ya kukagua ukarabati wa kiwanda hicho cha kuchakata samaki cha Alpha Tanganyika Flavour kilichopo wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa Agosti 13, 2020.

Akiwa katika kiwanda hicho, Dkt. Tamatamah alisema kuwa Rais Magufuli alipofanya ziara yake mwaka jana katika mkoa huo, moja ya maelekezo yake kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha kuwa katika mkoa huo kunaanzishwa kiwanda cha kuchakata samaki ili kuwaondolea kadhia ya masoko wanayoipata wavuvi wa maeneo hayo na mikoa ya jirani.

"Leo nimekuja na wataalamu wangu kukagua ukarabati unaoendelea katika kiwanda hiki cha Alpha ambapo ukikamilika na kiwanda hiki kuanza kazi kitatoa ajira zaidi ya mia moja(100) kwa wananchi na vile vile kitachangia kuongeza mapato ya Serikali,"alisema Dkt. Tamatamah

Dkt. Tamatamah aliendelea kueleza kuwa kiwanda hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuchakata Tani 20 za samaki ambazo bidhaa zake zitauzwa ndani ya Tanzania na vile vile katika soko la Marekani, hivyo kitasaidia nchi kupata fedha za kigeni.

Aidha, Dkt. Tamatamah alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo ya Alpha Tanganyika Flavour, Alpha Nondo kwa kuamua kufanya uwekezaji huo mkubwa ambao unatekeleza kwa vitendo agizo la Rais Magufuli huku akimuahidi kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kumpatia  ushirikiano utakaohitajika ili kumuwezesha kufikia adhma yake ya kuwekeza kiwanda hicho mkoani humo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji, Alpha Tanganyika Flavour, Alpha Nondo aliishukuru serikali kwa ushirikiano mkubwa wanaompatia huku akisema kiwanda hicho kitakuwa ni jibu kwa Rais Magufuli na Wavuvi waliokuwa wanahangaika na soko la kupeleka samaki wao.

"Kiwanda cha Alpha kinakuja kumkomboa mvuvi aliyekuwa hana uhakika na soko la samaki wake, hivyo nawaomba wavuvi na wananchi wote kutupa ushirikiano ili kiwanda hiki tunachoenda kukianzisha kiweze kuwahudumia vizuri,"alisema Nondo

Naye, Katibu Tawala Msaidizi, Mkoani Rukwa, Ocrani Chengula alisema kuwa kwa muda mrefu Mkoa huo ulikuwa unahangaika kupata kiwanda cha kuchakata samaki ili kiweze kuwasaidia wavuvi kupata masoko ya uhakika na kuachana na kufanya biashara ya kutorosha samaki kiholela katika nchi za jirani.

"Tunaamini kuanzishwa kwa kiwanda hiki kwanza kitatoa ajira kwa watu wetu hapa, lakini vile vile kitatuongezea mapato katika Halmashauri yetu na pia Wavuvi wetu wataachana na uuzaji holela wa samaki wao kwa sababu soko la uhakika litakuwa limepatikana kupitia Kiwanda hiki,"alifafanua Chengula

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi