Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Afrika Mashariki Wahimizwa Kutumia Bidhaa za Ndani
Dec 13, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma ametoa wito kwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kujivunia na kutumia bidhaa zinazozalishwa katika Jumuiya ili kuijenga Afrika Mashariki yenye uchumi stahimilivu na maendeleo endelevu. 

Waziri Riziki Pembe Juma ameeleza hayo alipokuwa akizungumza kwenye sherehe za SIKU YA TANZANIA (TANZANIA DAY) katika maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu kama “Juakali”, yanayoendelea katika viwanja vya Uhuru vya Kololo Jijini Kampala, Uganda. 

“Nimepata fursa ya kutembelea baadhi ya mabanda ya maonesho na nimefurahishwa kuona bidhaa mbalimbali kutoka kwa wajasiriamali, kwa kweli bidhaa zilizopo zina ubora na ubunifu na zinavutia sana. Nitoe rai kwa wana Afrika Mashariki kutumia bidhaa hizi zinazozalishwa katika Jumuiya ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kubadilisha sekta isiyo rasmi kuwa rasmi ili wananchi waweze kushiriki katika kuchangia maendeleo endelevu na pato la Jumuiya”. alisema Waziri Riziki Pembe Juma.

Maadhimisho ya TANZANIA DAY yaliambatana na shughuli mbalimbali zilizofanywa na wajasiriamali wa Tanzania kwa lengo la kusherehesha maonesho na kuonesha utamaduni wa Tanzania pamoja na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini. miongoni mwa shughuli zilizofanywa ni pamoja na maonesho ya mavazi ya asili, maonesho ya vito vya thamani na madini, vyakula vya asilia, ngoma za asili na muziki.  

Akizungumza na maelfu ya washiriki wa maonesho hayo Waziri Riziki Juma Pembe mbali na kutoa wito kwa wana Jumuiya kununua bidhaa za ndani alielezea hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kutatua changamoto zinazowakabili wajasiriamali, ambapo kwa upande wa Serikali ya Tanzania amezitaja hatua zilizochukuliwa kuwa ni pamoja na; kutoa mikopo yenye masharti nafuu, kuanzisha maeneo maaalum ya kufanyia biashara na kutoa elimu ya ujasiriamali.

“Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaendelea kuhakikisha wajasiriamali hawa hawaendelei kubaki wadogo bali wanapaswa kukua ili waweze kushiriki katika sekta rasmi kama wajasiriamali wakubwa. Vilevile kwa kushirikia na Sekretarieti ya Jumuiya tutahakikisha maonesho haya yanaendelea kufanyika kwa lengo la kuwapatia fursa wajasiriamali wa sekta hii ili waweze kutambua fursa zilizopo katika nchi zetu na kushiriki katika uzalishaji na maendeleo ya nchi zetu”. Alieleza Waziri Riziki Pembe Juma

Hii ni mara ya tano kwa Jamhuri ya Uganda kuwa mwenyeji wa maonesho haya tokea kuanzishwa kwake mwaka 1999.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi