Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 25 Novemba, 2022 amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.
Akiwa ziarani visiwani humo, Makamu wa Rais amefungua rasmi shule ya sekondari ya Ukerewe iliyopo kata ya Kagunguri iliyogharimu Shilingi bilioni 1.1 katika ujenzi wake.
Makamu wa Rais ameiagiza TAMISEMI kuhakikisha shule hiyo inawekewa miundombinu ya somo la fizikia ikiwemo maabara ya somo hilo ili iweze kukamilisha dhana ya sayansi. Pia Makamu wa Rais ameagiza ujenzi wa shule kuzingatia maendeleo ya sayansi na teknolojia ikiwemo kuweka miundombinu rafiki kwa masomo ya TEHAMA.
Akiwa shuleni hapo Makamu wa Rais amewasihi wazazi na walezi kusimamia watoto wao wapate elimu ili wawe msaada sahihi kwa maendeleo ya taifa. Amesema tatizo la mimba za utotoni limekua kubwa wilaya ya Ukerewe na hivyo kurudisha nyuma jitihada za Serikali katika kuboresha elimu wilayani hapo.
Makamu wa Rais amesema Serikali inaendelea na jitihada za kujenga miundombinu bora ya elimu pamoja na kutoa elimu bila malipo kwa elimu ya msingi na sekondari ili kuhakikisha taifa linapata wataalamu wenye tija.
Halikadhalika Makamu wa Rais amekagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Afya Igala kinachogharimu Shilingi milioni 492 katika ujenzi wake. Ameagiza kituo hicho kukamilika Disemba 20 mwaka huu na vifaa tiba kufungwa kabla ya kuisha mwezi februari 2023.
Akiwa katika kituo hicho cha Afya Makamu wa Rais amewasihi watendaji katika maeneo mbalimbali kuchukuwa kwa umuhimu suala la uhifadhi mazingira ikiwemo kupanda miti na kuifuatilia kwa manufaa ya taifa. Pia amewataka wananchi kutunza miundombinu ya kituo hicho cha Afya ili kiweze kutoa huduma kwa muda mrefu zaidi.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amezungumza na wananchi wa Wilaya ya Ukerewe katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Getrude Mongela.
Akihutubia katika mkutano huo, Makamu wa Rais amewaasa wananchi wa Ukerewe kujiepusha na vitendo vya uvuvi haramu unaopelekea uharibifu wa mazalia ya samaki na hivyo kuwa na upungufu wa samaki. Amewataka kufanya jitihada zaidi katika kulinda fukwe zinazozunguka kisiwa hicho pamoja na mazingira kwa ujumla.
Aidha. amesema Serikali imetenga kiasi cha fedha cha Shilingi bilioni 43 kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikubwa cha kupoza na kusambaza umeme katika kisiwa cha Ukerewe na ujenzi huo unatarajia kuanza Januari mwaka 2023 hivyo kukabiliana na changamoto ya kukatika umeme kisiwani humo.
Makamu wa Rais ameigiza TAMISEMI kwa kushirikiana vya vyombo vingine vya dola kudhibiti uvujaji wa mapato ya Halmashauri ya Ukerewe kupitia mawakala, wanasiasa na baadhi ya watumishi wasio waaminifu na wale watakaopatikana na hatia wachukuliwe hatua za kisheria haraka.
Pia amemuagiza Waziri wa Afya kuunda timu maalum ya uchunguzi kufuatilia mradi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Ukerewe ili kubaini mapungufu yaliopo katika matumizi ya fedha za ujenzi wa mradi huo.