Na Daudi Manongi, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi Mary Maganga amemwelekeza Msajili wa Hazina kutochambua bajeti yoyote itakayowasilishwa nje ya mfumo wa kielektroniki wa Planrep.
Bi Mary ameyasema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya Matumizi ya Mfumo Mpya wa Uandaaji na Uwasilishaji wa Bajeti na Taarifa za Bajeti ki-elektroniki wa PlanRep katika Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma jijini Dodoma.
“Ili kuwezesha ufanisi katika usimamizi wa mali za umma, ilihitajika pamoja na mambo mengine kuwa na mifumo madhubuti ya kielektroniki itakayorahisisha usimamizi wa rasilimali hizo”,alisema Bi Mganga.
Amesema hadi kufika mwezi Juni mwaka 2019, Serikali ilikuwa imewekeza katika Taasisi, Mashirika ya Umma na Kampuni zinazomilikiwa na Serikali kwa hisa chache zipatazo 266 zenye uwekezaji wa kiasi cha shilingi trilioni 59.6na kudhihirisha uhitaji wa mifumo ya kielektroniki.
Akieleza faida za mfumo huo, Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka amesema uwepo wa mfumo huu utasaidia kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za umma katika mashirika na taasisi za umma pamoja na upatikanaji wa taarifa za uhakika na kwa wakati; kupunguza gharama kubwa za fedha za umma katika ununuzi, uundaji, usimikaji, uendeshaji na usimamizi wa mifumo hiyo, pamoja kupunguza utitiri wa mifumo ya kibajeti ya kieletroniki iliyoanzishwa bila kupata ridhaa ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo ni msimamizi mkuu wa fedha na mali za umma.
Mafunzo hayo yatashirikisha jumla ya washiriki 944 kutoka katika taasisi na mashirika ya umma 236.