[caption id="attachment_46384" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi wa Idara ya Habari –MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi mbalimbali.[/caption]
Na Mwandishi Wetu
Ujenzi wa Barabara ya Njia Sita pamoja na barabara za waenda kwa miguu ya Kimara-Kibaha (Km19.2) wenye thamani ya TZS Bilioni 140.44 unaojumuisha madaraja ya Kibamba, Kiluvya na Mpiji umefikia 40%.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa Serikali, Mkurugenzi wa Idara ya Habari - MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa mradi huo unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia100 unaendelea kama ilivyopangwa na utakamilika kwa wakati.
Mradi huo unatarajiwa kuondoa changamoto ya foleni katika Jiji la Dar es Salaam hivyo kuchochea maendeleo na ukuaji wa uchumi.
“Serikali pia imesaini mkataba wa shilingi bilioni 699.9 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja refu zaidi Afrika Mashariki na Kati la Kilometa 3.2 kuunganisha mikoa ya Mwanza na Geita kwenye eneo la Kigongo-Busisi katika Ziwa Victoria”. Alisisitiza Dkt. Abbasi
Aliongeza kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Babaraba Vijijini na Mijini (TARURA) imejenga madaraja madogo madogo katika wilaya 7 nchini ambayo ni; Kondoa (Kisese, urefu mita 38, Bilioni 2.08); Kishapu (Manonga, urefu mita 45,Bilioni 2.436); Bahi (Chipanga Bridge, urefu mita 45, Bilioni 2.11; Iringa (M) (Tagamenda Bridge, urefu mita 30, Bilioni 4.5).
Madaraja mengine yamejengwa katika mikoa ya Songwe (W) (Kikamba Bridge, urefu mita 60, Bilioni 1.2); Iramba (Mtoa Bridge, urefu mita 60, gharama Bilioni 2.676 ); na Kilombero (Kihansi Bridge, Urefu mita 40, Gharama Milioni 972) “ Aliongeza Dkt Abbasi
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe magufuli imeweka mkazo katika kuimarisha miundombinu ili kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta mbalimabli ikiwemo uchukuzi, viwanda na kilimo.