Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Timu ya Wizara ya Kilimo Yatua Lindi na Mtwara Kuanza na Korosho, Waziri Hasunga Aongoza Msafara
Nov 13, 2018
Na Msemaji Mkuu

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe Evod Mmanda leo Novemba 13, 2018 mara baada ya kuwasili Mkoani humo kwa ziara ya kikazi kwa ajili ya kuhakiki Korosho zilizopo katika maghala makuu kabla ya kuanza ununuzi. 

Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo, Mtwara

Ikiwa ni siku moja tu mara baada ya kuapishwa kuongoza wizara ya kilimo katika hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam Jana Jumatatu Novemba 12, 2018, Waziri wa kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) Leo Tarehe 13 Novemba 2018 ameongoza viongozi wakuu wa Wizara yake kutembelea katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kwa ajili ya kuhakiki Korosho zilizopo katika maghala makuu.

Katika msafara huo Waziri Hasunga atatembelea Mkoani Mtwara ambapo ameambatana na Naibu Waziri wa kilimo Mhe Innocent Lugha Bashungwa na Katibu Mkuu Mhandisi Mathew Mtigumwe watakaotembelea Mkoa wa Lindi, na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo Prof Siza Tumbo atakayetembelea Mkoa wa Ruvuma.

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) akijadili jambo na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe Gelasius Byakanwa leo Novemba 13, 2018, mara baada ya kuwasili Mkoani humo kwa ziara ya kikazi kwa ajili ya kuhakiki Korosho zilizopo katika maghala makuu kabla ya kuanza ununuzi.

Katika ziara hiyo viongozi hao wakuu watahakiki usimamizi wa maghala ambao kwa sasa unasimamiwa naBodi ya usimamizi wa stakabadhi ya ghala na Usimamizi wa ziada wa Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko.

Vilevile watahakiki taarifa za Ubora wa maghala kama zilivyopitishwa na Bodi ya usimamizi wa Stakabadhi ya ghala (Warehouse Receipt Regulatory Board-WRRB) pamoja na Ubora wa ghala.

Watahakiki uwezo wa maghala na kiasi kilichopo ghalani, na kuhakikisha taarifa ya umiliki wa Korosho zilizopo kwenye ghala.

Naibu waziri wa kilimo Mhe Innocent Lugha Bashungwa (Mb) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi kwa ajili ya kuhakikisha Korosho zilizopo katika maghala makuu kabla ya kuanza ununuzi. Mwingine pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe Evod Mmanda, leo Novemba 13, 2018.

Kulia ni katibu Mkuu wa wizara ya kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe na Naibu Katibu Mkuu wizara ya kilimo Prof Siza Tumbo walipowasili Mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi kwa ajili ya kuhakikisha Korosho zilizopo katika maghala makuu kabla ya kuanza ununuzi leo Novemba 13, 2018.

Aidha, viongozi hao watahakiki kiasi cha Korosho kwenye ghala kwa kupitia nyaraka za mapokezi ya Korosho kwenye ghala ambazo zinawasilishwa na Vyama vya msingi (AMCOS) na kuoanisha taarifa hizo na taarifa zilizomo kwenye taarifa za stakabadhi ya ghala (Warehouse Report).

Katika ziara hiyo timu ya viongozi wakuu kutoka wizara ya kilimo wataambatana pia na Ofisini za Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Bodi ya Mazao Mchanganyiko, Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) - Naliendele, na Bodi ya usimamizi wa Stakabadhi ya ghala (WRRB).

 
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi