[caption id="attachment_34727" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati), akizungumza na mkandarasi anayejenga miundombinu ya kusambaza umeme kwa wananchi kupitia mradi wa Makambako hadi Songea, (kushoto) ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.[/caption]
Na: Zuena Msuya, Njombe
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amesema kuwa mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya kV220 kutoka Mji mdogo wa Makambako mkoani Njombe hadi Songea mkoani Ruvuma umekamilika na utazinduliwa muda wowote kuanzia sasa.
Dkt. Kalemani alisema hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua mradi huo katika Mji Mdogo wa Makambako mkoani Njombe, ambapo aliambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua na watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
[caption id="attachment_34728" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akikagua mradi wa njia ya kusambaza umeme kutoka Makambako hadi Songea.[/caption]Dkt. Kalemani alisema kuwa, kukamilika kwa mradi huo kutaokoa zaidi ya shilingi bilioni 9.1 zilizokuwa zikitumika kila mwaka kwa kununua mafuta mazito yaliyokuwa yakitumika kuzalisha umeme katika Mikoa ya Njombe, Ruvuma na Wilaya 8 zilizokuwa hazina umeme wa Gridi ya Taifa.
“ Kukamilika kwa mradi huu ambao ulianza mwaka 2016, kutaondoa adha na gharama ya kutumia mafuta mazito katika kuzalisha umeme kwa maeneo yaliyokosa umeme wa gridi ya taifa kwa miaka mingi ukiwemo Mkoa wa Ruvuma,” alisema Dkt. Kalemani.
Alisema kuwa, mashine tano zilizokuwa zikitumia mafuta mazito kuzalisha umeme zitazimwa, ili maeneo yaliyokuwa yakitegemea umeme huo wa mafuta mazito yaunganishwe katika gridi ya taifa.
[caption id="attachment_34729" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( katikati) akipata maelezo kutoka kwa Mkandarasi anayetekeleza mradi wa njia ya kusambaza umeme kutoka Makambako hadi Songea, wakati akikagua utekelezaji wa mradi huo ambao tayari umekamilika.[/caption]Alitaja maeneo yatakayounganishwa na gridi ya taifa kuwa ni pamoja na Mbinga, Madaba, Namtumbo, Njombe, Songea pamoja na Ludewa.
Dkt. Kalemani aliwataka wakandarasi wanaosambaza umeme katika maeneo yaliyopitiwa na mradi huo, kuharakisha uunganishaji wa wateja kwani tayari kuna umeme wa kutosha baada ya mradi huo kukamilika.
Aliwataka wakandarasi hao kuunganisha walau Vijiji vitatu kwa wiki ili kuendana na adhma ya Serikali ya kuunganisha vijiji vyote na huduma ya umeme ifikapo 2021.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, pamoja na kupongeza utekelezaji wa mradi huo, alimtaka Mkandarasi anayesambaza umeme katika Vijiji 122 katika mradi huo ambaye ni kampuni ya Isolux, kuhakikisha kuwa naye anakamilisha kazi aliyopewa ndani ya wakati aliopewa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Ally Kasinge ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, aliahidi kuwa viongozi wa Mkoa huo watasimamia ipasavyo utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya umeme kwa haraka.