Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mke wa Mwanri Ataka Wananchi Kuunga Mkono Juhudi za Viongozi
Dec 30, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Tiganya Vicent, RS TABORA

Wakazi wa Mkoa wa Tabora wametakiwa kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za viongozi mbalimbali mkoani humo katika kampeni za upandaji miti badala ya kuwakatisha tamaa kwa kuichoma moto na kuing’oa miti hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Tabora na Mke wa Mkuu wa Mkoa huo ,Bibi Grace Mwanri wakati wa zoezi la upandaji miti maji 500 iliyotolewa na Kampuni ya Usambazaji wa Gesi ya Manji’s kwa ajili ya kuungana na uongozi wa Mkoa wa Tabora katika kampeni ya kuifanya Tabora iwe ya kijana katika kipindi kifupi.

Alisema vitendo vya kuhujumu miti vinavyofanywa na baadhi ya wakazi wa Tabora kwa kuichoma na kuing'oa na wengine kuikanyaga na magari  vinaweza kuvunja moyo jitihada za viongozi wa mkoa huo.

Alisema kuwa ni vema wakazi wa Tabora wakatumbua miti sio ya Mkuu wa Mkoa au viongozi wengine bali ni kwa ajili ya faida ya jamii yote kwa ajili ya kuufanya Mkoa huo uwe wa kijani na mazingira yake yavutie watu kuishi.

 “Ni vema mtambue kuwa miti hii sio ya Mkuu wa Mkoa na wala sio ya viongozi bali ni ya wakazi wote wa Tabora…kwetu ni Moshi ipo siku tutaondoka na kurudi kwetu nyie ndio mtabaki mnanufaika na miti …hivyo ni vema kila mmoja achukue jukumu la kuilinda na kuwagombeza watu wote ambao wanaiharibu” alisema Mke huyo wa Mkoa.

Alisema kuwa hata Mwenyezi Mungu hapendezwi na watu wanaoharibu miti kwa kuichoma na kuing’oa kwani kufanya hivyo ni kutishia maisha watu wengine.

Bibi Grace alisema kuwa ni vema watu wachache wenye tabia hiyo ya kuiharibu miti wakafahamu kuwa miti hiyo imetumia pesa, nguvu, akili na muda katika kuiandaa na kuipanda na hivyo kuihujumu ni kusababisha hasara kwa jamii yote.

Kwa upande wa Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Nathalis Linuma alisema kuwa watumishi wote wa umma katika Mkoa wa Tabora waendelea kuunga mkono juhudi zilizosimamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora za kutaka katika kipindi kifupi kijacho eneo hilo liwe la kijani.

Alisema kuwa watumishi na wananchi zawadi pekee wanayoweza kumpa Mkuu huyo wa Mkoa ni kuhakikisha kuwa wanapanda miti kwa wingi na kuitunza ili kumtia moyo kwa juhudi zake alizianzisha.

Linuma aliwakumbusha kuwa juhudi hizo za Mkuu wa Mkoa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya viongozi wa juu ya upandaji wa miti kwa wingi kama sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na hivyo watumishi wote na wananchi wote wanatakiwa kushiriki kikamilifu na kwa nguvu zote.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi