Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Sipo Tayari Kumvumilia Mtumishi Mzembe-Nditiye
Oct 28, 2017
Na Msemaji Mkuu

Naibu Waziri wa Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akitoa maelekezo kwa Menejimenti ya Sekta ya Mawasiliano  wakati wa kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Wizarani mjini Dodoma alipowasili kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika nyadhifa hiyo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli 

Na. Mwandishi wetu

Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejikita kuwah udumia wananchi kwa wakati na inawataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii na haitamvumilia mtumishi wa umma yeyote ambaye ataonekana ni mkorofi na anakwamisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali. Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa kikao chake na Menejimenti ya Sekta ya Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo mjini Dodoma mara baada ya kuwasili    Wizarani hapo kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kushika dhamana ya kuongoza Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano ya Wizara hiyo. Mheshimiwa Nditiye amesema anawataka watumishi wa Sekta hiyo kuhakikisha kuwa wanafanyakazi kwa bidii, weledi wa hali ya juu na uaminifu ili rasilimali za Taifa zinufaishe wananchi na akaongeza kuwa “siko tayari kumvumilia mtumishi yeyote ambaye atakwamisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali”.

Kaimu Katibu Mkuu wa Sekta ya Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Anjelina Madete akimkabidhi Naibu Waziri wa Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara hiyo Mhandisi Atashasta Nditiye nyaraka mbalimbali zinazosimamia uendeshaji wa Sekta hiyo wakati wa kikao na Menejimenti ya Sekta hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Wizarani mjini Dodoma alipowasili kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika nyadhifa hiyo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli 

Ameitaka Menejimenti ya Sekta ya Mawasiliano kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Wizara ili wafahamu namna Serikali yao inavyowahudumia wananchi wake. Amesisitiza kuwa utendaji kazi ukiwa mzuri, mapato ya Serikali yanaongezeka na yataiwezesha Serikali kufikisha huduma mbalimbali kwa wananchi wake. Naibu Waziri huyo pia amewataka watumishi wa Sekta hiyo kutambua, kuzingatia na kujipanga kutekeleza majukumu yao kwa kulenga Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020, Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2017-2021 na kauli za viongozi wakuu wa Serikali ambazo ni maelekezo. Aidha, aliongeza kuwa ni muhimu kwa Sekta kushirikiana kwa karibu sana na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Miundombinu na wabunge wote ili kuhakikisha kuwa Serikali inapokea maoni yao kwa kuwa wao ni wawakilishi wa wananchi ili kuweza kuwahudumia wananchi hao. Mhe. Nditiye amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kumteua kwa kuwa wabunge wenye sifa na uwezo wako wengi ila amemuamini na kumpa dhamana ya kumsaidia kuongoza Sekta hizo. Pia, ameahidi kwamba hatamuangusha Mhe. Rais Dkt. Magufuli na Waziri wake, Prof. Makame Mbarawa na yuko tayari kutumikia wananchi kadri Mwenyezi Mungu atakavyopenda na kumjalia. Vile vile amesisitiza kuwa kwa msaada wa watendaji wakuu na watumishi wa Wizara ataweza endapo watampa ushirikiano wa kutosha. Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Sekta ya Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Anjelina Madete amesema kuwa Menejimenti na watumishi wanamkaribisha na wako tayari kumpa ushirikiano na hawatamuangisha ili wote kwa pamoja waweze kutumikia wananchi kuendana na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali Watu na Utawala wa Sekta ya Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Bi. Kitolina Kippa akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara hiyo Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa kikao na Menejimenti ya Sekta hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Wizarani mjini Dodoma alipowasili kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika nyadhifa hiyo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu wa Sekta ya Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Anjelina Madete.

Wakati akitoa taarifa ya utekelezaji na majukumu ya Sekta hiyo kwa Mhe. Nditiye wakati wa kikao hicho, Mhandisi Madete amesema kuwa Sekta imejenga miundombinu mbalimbali ya TEHAMA na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini kwa kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao unatoa huduma zake ndani na nje ya nchi, imejenga Kituo cha Taifa cha Data, kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Anwani za Makazi na Postikodi kwa kushirikiana na TAMISEMI, kufikisha huduma za mawasiliano vijijini kwa kuzipatia kampuni za simu ruzuku na kujenga minara, kuwezesha upatikanaji wa huduma mtandao kwa taasisi za Serikali na sekta binafsi na uwepo wa mifumo ya kielektroniki ambayo imeiwezesha Serikali kuongeza makusanyo ya kodi na mapato yake kwa ufanisi na kwa wakati hivyo kupunguza mianya ya rushwa na upotevu wa mapato ya Serikali. Katika hatua nyingine, Mhandisi Madete amempatia Mhe. Nditiye nyaraka mbalimbali zinazosimamia sekta ya Mawasiliano ikiwemo Sera, sheria na kanuni, Mpango Mkakati na hotuba ya Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/2018.  

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi