Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Selestine Kakele amesema zoezi la Mfumo wa Anwani za Makazi limekuwa na ufanisi mkubwa na kuwataka waratibu wa zoezi hilo wa mikoa kuendelea kukamilisha maeneo ambayo hayajafikiwa na mfumo huo.
Ameyasema hayo leo Agosti 21, 2023 mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Waratibu wa Anwani za Makazi wa Mikoa na Maafisa TEHAMA kutoka katika mikoa yote nchini na kuongeza kuwa mfumo huo mbali na ujenzi wa uchumi wa kisasa na utoaji wa huduma za kidigitali, pia una faida nyingi ikiwepo kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
"Mradi wa anwani za makazi mbali na ujenzi wake katika uchumi wa kisasa na utoaji wa huduma za kidigitali, pia una faida lukuki ikiwemo kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao,” amesema Bw. Kakele.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mulembwa Munaku amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza nguvukazi itakayosaidia katika kuimarisha utekelezaji na matumizi ya mfumo wa anwani za makazi sambamba na kuendeleza juhudi zilizoanzishwa kupitia Operesheni Anwani za Makazi.
“Operesheni hiyo ilizinduliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan Februari, 2022 ambayo ilifanikiwa kwa zaidi ya asilimia 95. Mafanikio hayo ndiyo yanayopewa kipaumbele katika kuyaendeleza na kuhakikisha kazi kubwa zaidi inafanyika kwa maslahi ya Watanzania,” amesema Bw. Munaku.
Nae Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bi. Zainab Hamis kibwana amesema zoezi la Anwani za Makazi ni la muhimu na kwamba ndilo litakaloiweka nchi katika ulimwengu wa kidigitali na kuipa heshima na hadhi ya miji ya Tanzania.