Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

ZIPA, TIC Zaagizwa Kuvutia Wawekezaji Hoteli Kubwa
Aug 29, 2023
ZIPA, TIC Zaagizwa Kuvutia Wawekezaji Hoteli Kubwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Hoteli iitwayo Kwanza iliyopo Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar tarehe 29 Agosti, 2023.
Na Mwandishi Wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuvutia wawekezaji wengi wa mahoteli makubwa, kutokana na ongezeko la watalii hapa nchini.

Mhe. Samia amesema hayo leo Agosti 29, 2023 wakati akifungua hoteli yenye hadhi ya Nyota Tano ya Kwanza Resort iliyopo Kizimkazi, Mkoa wa Kusini  Unguja, Zanzibar.

“Wito wangu kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuvutia wawekezaji wengi wa mahoteli makubwa, sababu wageni wanatuzidia,” amesema Mhe. Rais Samia.

Aidha ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, ambayo yanawavutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza Zanzibar.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa pamoja na Mmiliki wa Hoteli ya Kitalii iitwayo Kwanza, Bw. Hossam Elshaer kuashiria ufunguzi wa Hoteli hiyo iliyopo Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar tarehe 29 Agosti, 2023.

“Niwashukuru ndugu zangu wa Egypt kwa kuja kujenga hoteli hapa Kizimkazi. Aidha, mmiliki wa hoteli amesema yeye mwenyewe alikuja Zanzibar kutembea, na akavutiwa na mazingira ya Zanzibar, na akaamua kuja kujenga hoteli,” amesema Mhe. Rais.

Kwa upande wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Soraga amesema wamechukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya biashara, kuhakikisha wanafikia ufanisi unaotakiwa.

“Cheti cha uwekezaji kilikuwa kinatolewa miezi 3 hadi 6, lakini kwa sasa cheti hicho kinatolewa ndani ya masaa 24,” amesema Mhe. Soraga.

Aidha amesema kuwa, sera ya Uchumi wa Blue ipo katika mikono salama ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar  (ZIPA), Shariff A. Shariff amesema kuwa, Hoteli ya Kwanza ina vyumba 151, imeajiri watu 300, kati ya watu 300 walioajiriwa ni watu 10 tu wanatoka nje ya nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi