[caption id="attachment_43118" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwongeza wilayani Iramba, Mkoa wa Singida, alipokuwa katika ziara ya kazi Mei 17, 2019 kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na kuwasha umeme.[/caption]
Na Veronica Simba - Singida
Ziara ya siku mbili iliyofanywa na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani mkoani Singida, imeleta neema kwa wananchi wa Mkoa huo kutokana na hatua za kiutendaji alizochukua ili kuhakikisha miradi mbalimbali ya umeme inatekelezwa kwa kasi na viwango hivyo kuinufaisha jamii husika.
Katika ziara hiyo iliyofanyika Mei 15 na 16, 2019 ikilenga kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme mkoani Singida, Waziri alilazimika kutoa maagizo na hata kuchukua hatua za kinidhamu kwa watendaji kadhaa walioonesha kuzembea katika kutekeleza majukumu yao.
Akiwa katika kijiji cha Mwangeza wilayani Iramba, Mei 16, Waziri alitoa maagizo kwa Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa eneo husika, kuhakikisha ndani ya miezi sita kuanzia Mei 2019, umeme unashushwa na kuunganishiwa wananchi katika maeneo yote ambayo miundombinu ya umeme hususan nyaya zimepita.
“Viko vijiji vimepitiwa na nyaya za umeme lakini havina umeme. Natoa muda wa miezi Sita (6) kuanzia mwezi huu wa Mei, vyote viunganishiwe nishati hiyo.”
Vilevile, Waziri alitoa muda wa siku moja kwa uongozi wa TANESCO, kuunganisha umeme katika Jengo la Mahakama ya Mwanzo, lililopo katika Kata ya Mwangeza ili kuwezesha utoaji huduma bora kwa wananchi.
[caption id="attachment_43119" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akikagua utekelezaji wa miradi ya umeme kijijini Merya, Wilaya ya Singida Vijijini akiwa katika ziara ya kazi, Mei 16, 2019. Waziri aliagiza nyaya hizo za umeme zilizoachwa chini, zifungwe mara moja kwenye nguzo.[/caption]Aidha, akiwa katika kijiji cha Solya wilayani Manyoni, Waziri alitoa muda wa siku moja kwa uongozi wa TANESCO, kuunganisha umeme katika Mradi wa maji uliopo kijijini humo.
“Kwa kuwa vitendea kazi vyote vipo, ikifika kesho saa nane mchana, Mtambo huu wa maji uwe umeunganishiwa umeme, vinginevyo Meneja ujiuzuru wadhifa wako,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani akiwa kijijini Merya, Singida Kaskazini, alilazimika kutoa maagizo ya kukamatwa kwa baadhi ya Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme katika eneo hilo kutokana na kuzembea na kuidanganya serikali.
Wakandarasi waliokamatwa ni anayetekeleza Mradi wa Backbone ambaye Waziri alisema muda wa mkataba wake umeisha lakini bado hajakamilisha kazi yake. Pamoja na kuagiza akamatwe ili ahojiwe, lakini pia alimtaka kuhakikisha anakamilisha kazi iliyobaki ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Mwingine ni anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II), ambaye pia, kwa mujibu wa Waziri amezembea, haonekani katika eneo la kazi na ametelekeza nguzo takribani miezi Tisa (9) pasipo kuzifungia nyaya.
Akifafanua zaidi, Waziri alisema Mkandarasi wa REA II ameidanganya serikali, hajakamilisha kazi takribani miezi minne sasa. “Alitakiwa akamilishe kazi Desemba mwaka jana, lakini hadi sasa bado na hayuko site.”
Kufuatia hatua hiyo, Waziri Kalemani alitoa onyo kwa wakandarasi wengine nchi nzima wanaotekeleza miradi mbalimbali ya umeme kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo vinginevyo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Pia, Waziri alimwagiza Meneja wa TANESCO Mkoa wa Singida, kumwondolea wadhifa wa Msimamizi wa Miradi ya REA, Fundi Mchundo kutoka shirika hilo, aliyekuwa akishikilia wadhifa huo kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kumweka Afisa mwingine.
[caption id="attachment_43120" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (mwenye shati la bluu-kushoto), akijionea shughuli za ujasiriamali wa kuchomelea vyuma zinazofanywa na kikundi cha vijana wa kijiji cha Merya, wilayani Singida Vijijini, akiwa katika ziara ya kazi, Mei 16, 2019. Mradi huo wa vijana ni matunda ya upelekaji huduma ya umeme uliofanywa na serikali katika eneo hilo kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA).[/caption]Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani aliwasha umeme kwenye vijiji mbalimbali katika Wilaya za Manyoni, Iramba na Mkalama pamoja na kuzungumza na wananchi.
Alipongeza taasisi mbalimbali za umma, zikiwemo shule, vituo vya afya, ofisi za kata na vijiji, miradi ya maji na nyinginezo ambazo zimefanya jitihada ya kulipia shilingi 27,000 tu na kuunganishiwa umeme ambapo alitoa hamasa kwa taasisi nyingine nchi nzima kuiga mfano huo.
Alisema, kipaumbele cha serikali katika kuunganisha umeme vijijini ni katika taasisi zinazotoa huduma mbalimbali kwa umma hivyo akawataka viongozi wote wanaohusika, kuhakikisha wanatenga fedha za kulipia taasisi zao ili ziunganishiwe umeme.
Aidha, alitoa hamasa kwa wananchi kuchangamkia miradi ya umeme vijijini kwa kulipia gharama ndogo kiasi cha shilingi 27,000 ili waunganishiwe umeme katika makazi yao na biashara zao.
Pia, aliwataka kuutumia umeme katika kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuongeza kipato na kujiinua kiuchumi.
Katika ziara hiyo, Waziri aliambatana na viongozi mbalimbali wa serikali na kisiasa wakiwemo Wakuu wa Wilaya husika, Wabunge wa maeneo husika na wataalamu kutoka wizarani, TANESCO na REA.